Polisi katika Kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya wameanzisha uchunguzi baada ya kugundulika kuwa mwanaume mmoja alianzisha kituo bandia cha doria ya polisi eneo la Cherus, bila idhini wala ujuzi wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Citizen Digital, mshukiwa huyo, Collins Leitich, anayejulikana pia kwa jina la utani Chepkulei, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Asis, eneo la Ndugulu, aliamua mwenyewe kuanzisha kituo hicho kwenye jengo moja. Alienda mbali zaidi kwa kukipaka rangi rasmi za polisi, akitoa taswira ya kituo halali cha usalama.
Kituo hicho bandia kiligunduliwa na maafisa wa serikali za mitaa, ambao mara moja walitoa taarifa kwa polisi ambao walianzisha uchunguzi. Wakazi wa eneo hilo wameelezea mshtuko wao baada ya kugundua kuwa kituo hicho hakikuwa halali.
"Tulishangazwa kujua kuwa kituo cha doria kilichopo hapa hakikuwa rasmi. Wengi wetu tulidhani ni juhudi halali za kuboresha usalama katika eneo hili," alisema mmoja wa wakazi.
Hata hivyo, mamlaka bado haijabaini nia ya mshukiwa katika kuanzisha kituo hicho bandia. Polisi wamewahakikishia wakazi kuwa hatua stahiki zitachukuliwa huku uchunguzi ukiendelea.