Rais wa Rwanda Paul Kagame na Félix Tshisekedi wa DR Congo wamekutana mjini Doha, Qatar na kukubaliana kuendelea na mazungumzo kuhusu amani ya kudumu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ilisema.
Kagame na Tshisekedi walikutana mara ya mwisho ana kwa ana kuhusu suala hilo Septemba 2022 mjini New York wakipatanishwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Majaribio kadhaa ya wapatanishi wengine kuwaleta viongozi hawa pamoja katika juhudi za amani yameshindwa tangu wakati huo.
Mkutano na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, unaonyesha dhamira ya nchi hiyo na maslahi ambayo DR Congo na Rwanda walinayo katika uhusiano wao na Qatar.
Viongozi hao pia walikubali kuendelea kutafuta amani kupitia “mazungumzo mapya na yaliyoratibiwa ya Luanda/Nairobi”, kulingana na taarifa ya wizara.
Umoja wa Mataifa, DRC na baadhi ya nchi za Magharibi zinaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa M23. Katika siku za hivi karibuni haijakanusha moja kwa moja au kukiri.
Mkutano huo wa Doha ulifanyika huku kukiwa na ripoti za mapigano Jumanne katika eneo la Walikare kati ya M23 na upande wa vikosi vya serikali.
Dk.Mohammed Al-Khulaifi Waziri wa Serikali anayehusika na upatanishi na utatuzi wa migogoro aliambia mtandao wa X kwamba Qatar inathibitisha kwamba mazungumzo ndiyo njia halisi ya kusuluhisha tofauti kati ya nchi na kufikia amani.