Rais wa Urusi, Vladimir Putin amekataa kusitisha vita kwa ujumla nchini Ukraine, akiridhia tu kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati baada ya mazungumzo yake na Rais wa Marekani, Donald Trump. Putin amekataa kutia saini mpango wa kusitisha vita kwa mwezi mmoja, uliokubaliwa hivi karibuni kati ya timu ya Trump na Ukraine nchini Saudi Arabia, akisisitiza kuwa makubaliano ya kina yanawezekana tu ikiwa msaada wa kijeshi wa kigeni kwa Ukraine utasitishwa.
Kituo cha habari cha BBC kinaripoti kuwa masharti hayo yamekataliwa na washirika wa Ulaya wa Ukraine, huku Marekani na Urusi zikiendelea na mazungumzo yanayotarajiwa kuendelea Jumapili huko Jeddah, Saudi Arabia. Mjumbe wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, amesema kuwa licha ya Putin kukataa makubaliano mapana, pande zote zimekubali kuendelea na mazungumzo zaidi ya amani.
Katika vita hivyo vinavyoendelea kwa mwaka wa tatu sasa, Urusi hivi karibuni ilifanikiwa kurejesha udhibiti wa eneo la Kursk, ambalo lilikuwa limetekwa na vikosi vya Ukraine miezi sita iliyopita.
Matokeo ya mazungumzo hayo yanaashiria mabadiliko katika msimamo wa Marekani, ambayo wiki moja iliyopita ilionekana kusisitiza usitishaji vita wa haraka. Hata hivyo, Trump na Putin wamekubaliana kuwa mazungumzo ya amani yataendelea mara moja katika Mashariki ya Kati.
Wakati wajumbe wa Marekani walipokutana na wenzao wa Ukraine mjini Jeddah, walishinikiza Kyiv kukubali pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku 30 ardhini, angani na baharini.
Baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati ya Trump na Putin, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, aliwasili Helsinki, Finland, kwa ziara rasmi na kusema kuwa Ukraine iko tayari kwa mazungumzo ya kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati lakini inahitaji maelezo zaidi kuhusu makubaliano hayo.
Aidha, Zelensky alimshutumu Putin kwa kuendelea na mashambulizi, akidai kuwa Urusi imefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika maeneo mbalimbali, ikiwemo hospitali ya Sumy na miundombinu ya umeme huko Sloyansk.