Mkongwe wa filamu nchini Steven Nyerere, ameamua kuvunja ukimya na kutoa ushauri juu ya mchezo wa Kariakoo Derby nini kifanyike ili Derby hiyo ifanikiwe kuchezwa.
Steve Nyerere ameeleza kuwa Rais Samia akipenda kwenda kuangalia Derby pale uwanja wa Taifa, pamoja na watanzania na mashabiki wa Simba na Yanga itapendeza sana. Ana Imani kuwa timu zote zitafurahia kuazimisha miaka minne ya Rais wetu mpendwa kwa kucheza Derby. Maana ndani ya miaka minne ya Rais Samia, soka limekuwa kivutio kikubwa sana na muamko wa soka umekuwa mkubwa baada ya Rais Samia kuhakikisha sekta hii inapiga hatua.
Steve ameongeza kuwa kuazimisha miaka minne ya kipenzi cha watanzania Dr. Samia Suluhu Hassan Derby halafu mgeni rasmi ni mama Samia itapendeza na watu watajaa balaa. Haya yote yanajiri mara baada ya mashabiki wa timu zote mbili (Simba na Yanga) kutoelewa muafaka wa mchezo huu ambao ulikuwa ufanyike tarehe 8 Machi.
Mchezo huo ulihairishwa kutokana na timu ya Simba kugoma kupeleka wachezaji wake uwanjani, kwa kudai kuvunjiwa sheria ya kutoruhusiwa kuingia uwanjani kufanya mazoezi ikiwa imebaki siku moja mchezo huo ufanyike. Utakumbuka mnamo tarehe 7 Machi mida ya saa moja jioni, Simba wakiwa na gari lao walikwenda kwa Mkapa, baada ya kufika walizuiliwa kuingia na watu waliojiita makomandoo wa Yanga.
Wachezaji wa Simba waliamua kuondoka na baada ya muda walichapisha barua iliyoeleza kwamba, hawatashiriki mechi ya Kariakoo Derby kutokana na kuzuiliwa kuingia uwanjani. Japo bodi ya ligi ilitoa tamko hakuna mechi kuhairishwa, lakini Simba walibaki na msimamo wao na hatimaye bodi ya ligi kuu Bara iliridhia mchezo huo kuhairishwa.
Hapa majuzi kilifanyika kikao baina ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na michezo Mh. Kabudi na viongozi wa timu zote mbili pamoja na viongozi wa bodi ya ligi kuu bara, lakini mpaka kikao hicho kinamalizika hakuna muafaka uliopatikana juu ya mchezo huo urudiwe siku gani. Je maoni ya Steve Nyerere kudai Rais Samia awe mgeni rasmi katika mchezo wa Derby yatasaidia timu zikubali kucheza mechi hiyo?
Chanzo; SamMisago Tv.