Web

TANZIA:Msanii G San wa X Pllastaz Afariki Dunia

TANZIA:Msanii G San wa X Pllastaz Afariki Dunia


Jamii ya hip hop nchini Tanzania ipo katika majonzi kufuatia kifo cha msanii mahiri wa muziki huo na member wa kundi kongwe la X Plastaz, G San.

G San amefariki dunia March 23, akiwa Chicago, Illinois, Marekani, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia na vyanzo vya karibu.

Chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika.

G San alijulikana zaidi kupitia kundi la X Plastaz, maarufu kwa kuchanganya muziki wa hip hop na utamaduni wa Kimaasai, akiwa mmoja wa waasisi waliotoa sauti za kipekee kwa kizazi kipya cha muziki wa Tanzania.

Mwaka 2009, G San aliweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kushiriki kwenye BET Hip Hop Awards Cypher, akitumbuiza bega kwa bega na wasanii wakubwa wakiwemo KRS-One, Nipsey Hussle, na Wale. Uwakilishi wake kwa lugha ya Kiswahili uliwavutia wengi, wakiwemo wakali wa muziki huo kama DJ Premier.

“Kwangu ilikuwa ni heshima kubwa kuwa jukwaa moja na wakali kama Eminem na KRS-One. Niliimba kwa Kiswahili na waliniuliza kwa nini—nikawaambia Kiingereza siyo lugha yangu ya kwanza,” alisema G San wakati huo.

G San na X Plastaz walitoa vibao maarufu kama Bamiza, Aha!, Dunia Dudumizi na Nini Dhambi kwa Mwenye Dhiki, wimbo ambao video yake ilirekodiwa juu ya mlima Ol Doinyo Lengai, na kuwa moja ya video maarufu zaidi za muziki wa Afrika Mashariki kwenye YouTube.

Kifo cha Father Nelly, mmoja wa waanzilishi wa X Plastaz mwaka 2006, kilikuwa pigo kubwa, lakini G San aliendeleza harakati kwa kutumia muziki kama chombo cha kupigania haki za jamii na kutangaza utamaduni wa Kiafrika.

Mipango inaendelea ya kusafirisha mwili wa G San kwenda Arusha kwa mazishi, ambako familia yake imethibitisha kuwa taratibu zote zinawekwa sawa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad