Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “JUDE” katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo imeeleza uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa inaonesha kimbunga hicho kitaingia nchi kavu katika eneo la Msumbiji leo na kupungua nguvu yake.
Hata hivyo, Kimbunga “Jude” kinatarajiwa kurejea tena baharini na kuimarisha nguvu yake katika kipindi cha kati ya Machi 13 hadi 15 2025.
Aidha, kutokana na mwelekeo na umbali wake Kimbunga “Jude” hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja hapa nchini. Hata hivyo, uwepo wa kimbunga hicho katika eneo la Rasi ya Msumbiji unatarajiwa kuchagiza mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali.