Serikali imesema kuwa inaendelea na mpango wa kununua umeme kutoka nje ya nchi kwa ajili ya Kanda ya Kaskazini ili kupunguza upotevu mkubwa wa umeme unaosababishwa na usafirishaji wa nishati hiyo kutoka Gridi ya Taifa, hali inayosababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 32 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari – MAELEZO na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, umeme uliopo kwenye Gridi ya Taifa unazalishwa zaidi katika Ukanda wa Kusini Mashariki, hivyo hulazimika kusafirishwa umbali mrefu hadi Kanda ya Kaskazini, jambo linalosababisha upotevu mkubwa wa nishati hiyo.
“Kwa sasa, upotevu wa umeme unaosafirishwa kuelekea Kanda ya Kaskazini unasababisha hasara kubwa kwa Taifa, na moja ya njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo ni kununua umeme kutoka Ethiopia kupitia Kenya,” imesema taarifa hiyo.
Imeelezwa kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Kanda ya Kaskazini na kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.
Serikali pia imeeleza kuwa gharama za umeme unaonunuliwa kutoka Ethiopia ni nafuu zaidi kutokana na Tanzania kuwa mwanachama wa Gridi ya Umeme ya Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika, ambapo nchi wanachama huuziana umeme kwa gharama za chini ikilinganishwa na gharama za uzalishaji wa ndani kwa baadhi ya vyanzo vya nishati.
Aidha, imefafanua kuwa utaratibu wa Tanzania kununua umeme kutoka nchi jirani si jambo jipya, kwani umekuwa ukifanyika kwa miaka mingi katika mikoa ya pembezoni kama vile Rukwa (kutoka Zambia), Kagera (kutoka Uganda), na Tanga (kutoka Kenya).
Serikali imeeleza kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuimarisha Gridi ya Taifa na kuwezesha nchi kuwa na njia mbadala ya kupata umeme pale kunapotokea changamoto katika uzalishaji wa ndani.
Hatua hii pia inaendana na makubaliano yaliyofikiwa na Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki katika Mkutano wa Nishati uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, ambapo walikubaliana kuunganisha gridi za nchi zao ili kurahisisha biashara ya umeme na kuboresha upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi.