Web

Tuzo za Trace zilivyoacha Maswali Mengi Bila Majibu


Akilini mwangu nilikuwa naona kwamba muziki wa Bongo umevuka mipaka hasa ukizingatia channel hiyo haikuwa inarusha matangazo kutoka Bongo.

Zanzibar. Kila nikifumba macho unanijia usiku wa tuzo za muziki za Trace 2025, zilizofanyika wiki iliyopita Zanzibar. Pia nakumbuka miaka ya nyuma, nilivyokuwa nafurahi kuona ngoma za wasanii wa Bongo zikioneshwa kwenye channel ya Trace Mziki.

Akilini mwangu nilikuwa naona kwamba muziki wa Bongo umevuka mipaka hasa ukizingatia channel hiyo haikuwa inarusha matangazo kutoka Bongo.

Si haba siku zilivyozidi kwenda Trace Music ambao ni sehemu ya Trace Group, kampuni ya kimataifa inayojihusisha na vyombo vya habari, burudani, na tamaduni za vijana, hasa barani Afrika na katika jamii za watu weusi duniani kote. Wakaona kuna haja ya kuja na tuzo za muziki.


Ndipo mwaka 2023, wakaja na Trace Awards & Festival kwa lengo la kusherehekea maadhimisho ya miaka 20 ya kituo hicho cha televisheni cha muziki cha kulipia cha Ufaransa, Trace TV.


Hapo ndipo toleo la kwanza la tuzo hizo likafanyika Oktoba 21, 2023. Katika BK Arena, Kigali, Rwanda. Katika tamasha hilo mambo yalikuwa poa sana, naweza kusema ilikuwa fungua dimba ya kibabe.


Nakumbuka katika usiku huo wasanii kama Burna Boy (Nigeria), Rema (Nigeria), Diamond Platnumz (Tanzania), Yemi Alade (Nigeria), Davido (Nigeria), Viviane Chidid (Senegal), Roseline Layo (Ivory Coast), Fally Ipupa (DRC) na wengineo waliondoka na tuzo.


Haikuishia hapo utamu wa tuzo hizo ulizidi baada ya kutangazwa kuwa zitafanyika Zanzibar kwa mwaka 2025. Siku hazigandi kweli kuanzia Februari 24-26, 2025. Tanzania ikaitika ujio wa tuzo hizo Kisiwani Unguja. Wasanii nao kutoka mataifa mbalimbali walishuka kushuhudia ugawaji wa tuzo hizo. Na haya ndiyo yalitokea.


Hapa Trace waliupiga mwingi

Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Kila nilipokuwa naangalia vipengele vya washindani katika tuzo hizo, nilikuwa natamani usiku huo ufike haraka ili nishuhudie nani ataondoka na tuzo. Hata nilipokuwa kwenye porojo na marafiki nao tamaa yao ilikuwa hiyo hiyo.

Hiyo ilinipa picha ya kuwa mtanange haukuwa wa kitoto, kila msanii alionekana anajua zaidi ya mwenziye hivyo hata mimi nilichanganyikiwa kila nilipokuwa nabashiri atayekuwa mshindi. Kwa hili Trace hongerani.  

Aidha kwenye upande wa orodha ya watumbuizaji nayo ilikaa kibabe. Ilionesha kutakuwa na burudani isiyochosha. Na kubwa zaidi ni yale madarasa ya wasanii kuchangia ujuzi wao wa namna gani ya kupiga pesa kupitia muziki.

Katika madarasa hayo yaliyoanza Februari 24 hadi 25 kabla ya 26 usiku wa tuzo. Wasanii kama Zuchu, Diamond, Yemi Alade na wengine walichangia uzoefu wao hii ina maana kubwa kwenye biashara ya muziki. Kwa hili pia Trace mliupiga mwingi, hasa ikizingatiwa kwa sasa muziki si sehemu ya kuburudika tu bali ni sehemu ya kujipatia kipato pia.

Haya yasijirudie

Licha ya kuwepo kwa mazuri katika usiku huo. Lakini kitumbua kiliingia mchanga baada ya Trace kutangaza uwepo wa upepo mkali kisiwani hapo, hivyo muda wa kuanza tamasha utasogezwa mbele.

“Kwa sababu ya upepo mkali, Shindano la Trace sasa litaanza saa:

Blue Carpet – Saa 6:30 PM GMT // 7:30 PM WAT // 9:30 PM EAT  

 Tuzo – Saa 8:00 PM GMT // 9:00 PM WAT // 11:00 PM EAT,” ilieleza taarifa yao waliyoiweka kwenye ukurasa wao wa Instagram.



Hii inatoa funzo la kuzingatia na kufuatilia Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kila inapotoa maelekezo. Hasa wakati wa kuandaa matamasha makubwa kama hilo. Kwani tangu Januari TMA ilitoa tahadhari kwa badhi ya maeneo na Zanzibar ikiwemo.

Hata hivyo licha ya tangazo hilo ‘Blue Carpet’ katika usiku huo ilianza saa 3:30 usiku. Huku kwa waliokuwa wakitazama kupitia runinga na mtandaoni, kulitawaliwa na matangazo ya muda mrefu.

Kusogezwa mbele kwa tamasha hilo naweza kusema ndiyo chanzo cha majanga yote hayo. Kwani kila kitu ilibidi kiende haraka ili kukimbizana na muda. Lakini bado haikusaidia kitu badala yake iliharibu kabisa.


Nilitegemea usiku ule kuona mastaa mbalimbali wakikatiza kwenye Blue Carpet wakionesha namna ambavyo wamependeza, lakini mambo hayakuwa hivyo wachache sana ndiyo walionesha mavazi yao, kisha kamera zikahamia ndani kwenye tukio husika.


Huko ndani sasa. Mwonekano wa jukwaa haukuwa wa hadhi ya Trace yaani ilikuwa kawaida sana. Matarajio ya mashabiki wengi yalikuwa ni kuona wasanii wakitumbuiza kwa muda wakutosha.


Lakini mambo hayakuwa hivyo. Baadhi ya wasanii walitumbuiza kwa dakika chake kisha kushuka, inawezekana yalikuwa ni makubaliano yao. Lakini kwa waliofuata burudani hawakukatwa kiu yao.


Wapo mashabiki waliofunga safari kutoka mataifa mbalimbali, wakifuata burudani Tanzania. Lakini waliishia kutazama nusu ya utumbuizaji huku msanii kama Alikiba akiondika bila kutumbuiza. 


Achana na hilo, ugawaji wa tuzo nao haukupangwa katika mtiririko mzuri. Hadi saa nane usiku ni vipengele vitatu tu ndiyo vilivyokuwa vimetangazwa. Hii siyo sawa. Na mbaya zaidi ni pale ambapo matangazo ya moja kwa moja yalipokata kila sehemu ambapo tamasha hilo lilikuwa likioneshwa. Yaani kuanzia YouTube hadi kwenye Channel zote za Trace.


“Kwa sababu ya shida za kiufundi, miongoni mwa matangazo yetu ya moja kwa moja. Tulilazimika kukatiza matangazo hayo katika YouTube na vituo vyote vya televisheni,”ilieleza taarifa ya pili iliyotolewa na Trace.


Hii ilionyesha udhaifu mwingine kwa tamasha hilo. Kwani kwa ukubwa wake suala la shida ya kiufundi lilitakiwa kudhibitiwa mapema hasa katika siku kubwa kama hiyo ya ugawaji wa tuzo. 


Hata hivyo, baada ya kukosea wengi walitegemea kupata kila kilichoendelea katika kurasa ya Instagram ya Trace lakini pia haikuwa hivyo. Hadi kumalizika kwa tamasha hilo wengi walikuwa hawaelewi nani kashinda nani hajashinda. Hapa pia Trace mlikosea. 





Inapotokea shida kama hiyo ni vyema kuwapa yanayojiri mashabiki hata kupitia kurasa zenu za mitandao ya kijamii, kwa haraka iwezekanavyo ili kutowaacha njia panda. Taarifa za kuomba radhi pekee hazitoshi. Kwa ufupi waandaaji wa Trace 2025 mnapaswa kujifunza kutokana na makosa ili mambo yasije kujirudia kwa wakati mwingine. 


Ikumbukwe kuwa Trace ilianzishwa mwaka 2003 na Olivier Laouchez, mfanyabiashara wa Kifaransa mwenye asili ya Martinique. Alianza kama kituo cha televisheni kinachojikita kwenye muziki wa Hip-Hop, R&B, na Afro-urban.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad