Mwaka 2004, Mfanyabiashara Mwandishi wa Vitabu, Eric James Shigongo, alianzisha Shindano la kumtafuta Mkali wa kughani muziki wa Rap nchini. Shindano hilo aliliita "Mfalme wa Rhymes 2004".
Kupitia Kampuni ya Global Publishers iliyokuwa ikichapisha magazeti ya Kiu, Uwazi na Ijumaa, Shigongo akatangaza mchakato wa kuwapata washiriki wa shindano hilo.
Ndani ya magazeti hayo kukawa na sehemu ya 'Coupon', ambayo msomaji alitakiwa kupendekeza wasanii 10 na nyimbo anazotaka ziingie kwenye shindano.
Baada ya kuchagua, msomaji atatakiwa kukata Coupon na kuituma kupitia anuani iliyowekwa, na baadae washiriki waliopendekezwa zaidi watatangazwa.
Nyakati hizi hazikuwa za mitandao ya kijamii, hivyo magazeti mengi yalitumika kuandika na kuhamasisha mambo mengi yanayohusu michezo, sanaa na burudani.
Kampuni ya kuuza magari nchini ya Conti-Car Sales, ikajitosa kudhamini Shindano hilo na kutoa zawadi ya gari ndogo aina ya 'Toyota Sera' kwa Mshiriki atakayetangazwa kuwa mshindi.
Joto la Shindano hilo likaifunika, Magazeti ya Shigongo yakauzwa kama njugu, Wasomaji wengi wakagombea kuyanunua kwa ajili ya kukata Coupon ili kuchagua wasanii wanaowataka.
Hatimaye mchakato ukakamilika ndani ya siku 30. Kampuni ya Global Publishers ikatangaza wasanii 10 waliopendekezwa zaidi kushiriki mashindano hayo sambamba na nyimbo zilizopelekea wao kuchaguliwa.
Wasanii waliopendekezwa kushiriki Shindano hilo na nyimbo zao ni, Profesa Jay (Usinitenge), Soggy Doggy (Kibanda Cha Simu), Afande Sele (Mtazamo), Jay Moe (Mvua na Jua) na Mwana FA (Alikufa kwa Ngoma).
Wengine ni Dully Sykes (Salome), Mandojo na Domokaya (Nikupe Nini) Solo Thang (Simu Yangu), Inspekta Haroun (Kisa Cha Baba Mkwe), na Ferooz (Mkasa wa Bosi).
Hata hivyo, siku chache kabla ya Shindano hilo kufanyika, Msanii Dully Sykes akatangaza kujitoa kushiriki Shindano hilo kwa sababu ambazo hakuwa tayari kuziweka wazi.
Wasanii wote wakaitwa kwenye semina kuelezwa utaratibu utakavyokuwa siku ya shindano hilo, kwamba kwanza watatakiwa kuimba nyimbo 3 badala ya wimbo 1 uliochaguliwa na wasomaji.
Wakaelezwa kuwa, baada ya mzunguko wa kwanza wa kila msanii kuimba wimbo uliopendekezwa, utafuata mzunguko wa pili wa msanii kuimba wimbo wa pili ambao atauchagua yeye mwenyewe.
Waratibu wakendelea kuwaeleza washiriki wa Shindano hilo kuwa, baada ya mzunguko wa pili kwisha, Majaji watatangaza wasanii walioingia kwenye hatua ya Tano Bora.
Wasanii waliofanikiwa kutinga 'Top 5' watatakiwa kuimba wimbo mmoja mmoja wa mwisho ambao wameuchagua wao wenyewe, kabla ya Jaji mkuu kumtangaza mshindi wa shindano hilo.
Hatimaye siku ikafika. Ukumbi wa Diamond Jubilee ukafurika isiyo mfanowe. Mimi (Kado Cool) nikiwa meza ya mbele kabisa, pembeni ya Mshindi wa Pili wa Miss Tanzania 1994, Tabasamu Ngongoseke.
Uratibu wa washiriki kupanda jukwaani ukawa 'Kosa la Kwanza' binafsi kulibaini kwenye Shindano hilo. Waandaaji wakakosea kupanga mwanzoni nyimbo zilizoshirikisha wasanii wanaoshiriki shindano hilo.
Baadhi ya wasanii wakalazimika kupanda jukwaani kuimba nyimbo walizoshirikishwa, kabla ya zamu yao ya kutakiwa kupanda ili kuimba nyimbo zao kama washriki wa shindano hilo.
Hatua hii ikachangia sana kupunguza mvuto wa msanii ambaye ameshatokea jukwaani kuimba wimbo aliishirikishwa, kabla ya zamu ya kutakiwa kuimba wimbo wake kufika.
Mfano, msanii Ferooz, alipangwa mapema kuimba wimbo wake wa 'Mkasa wa Bosi' ambao amewashirikisha Juma Nature na Solo Thang, ilhali Solo akiwa mshiriki wa Shindano hilo.
Tokezo la mapema la Solo kabla ya zamu yake kufika, lilipunguza mno mshamsham alipokuja kuimba wimbo wake wa 'Simu Yangu', kwani mashabiki hawakulipuka, kwa sababu walikuwa tayari wameshamuona.
Hali kama hiyo ikawakuta pia Jay Moe na Soggy Doggy ambao walishiriki kuimba wimbo wa "Simu Yangu" wa Solo Thang, na hivyo hata baada ya kupanda kuimba nyimbo zao, hawakupata mapokeo mazuri kwa sababu 'walishaonwa'.
Baada ya wasanii wote kumaliza kuimba mizunguko yao miwili, muda wa kutaja wasanii waliofanikiwa kuingia 'Tano Bora' ukawadia. Ukumbi wote ukawa kimya, huku kila mtu akisubiri kwa hamu kusikia msanii yupi na yupi aliyefanikiwa kupenya.
Jaji Mkuu, Taji Liundi akapanda Jukwaani kuwatangaza Mwana FA, Ferooz, Mandojo na Domokaya, Inspekta Haroun, na Afande Sele kuwa wameingia 'Tano Bora' na Wasanii Profesa Jay, Solo Thang, Jay Moe, na Soggy Doggy kuwa wametupwa nje ya shindano hilo.
Matokeo hayo ya 'Top 5' yakapokelewa kwa hisia tofauti sana ukumbini. Baadhi ya mashabiki walishanglia, lakini baadhi walioneshwa kuchukizwa na 'Vigogo' kutupwa nje ya shindano hilo, na hivyo kuamua kuondoka ukumbini kwa hasira.
Hata baada ya mzunguko wa mwisho kwa wasanii hao kwisha na kisha Jaji Mkuu Taji Liundi kupanda Jukwaani na kuwatangaza Afande Sele kuwa mshindi, ukumbi uliendelea kugawanyika kwa matabaka, ilhali wengine wakishangilia, huku wengine wakizomea.
Afande Sele akatangazwa rasmi kuwa "Mfalme wa Rhymes 2004" akifuatiwa nyuma na Inspekta Haroun aliyeshika nafasi ya 2, Mandojo na Domokaya wakiwa nafasi ya 3, Ferooz nafasi ya 4, na Naibu Waziri Mwana FA akiburuza mkia kwenye nafasi ya 5.
Huu ukawa mwanzo wa enzi, na mwisho wa enzi. Enzi Mpya ya Bifu kali kati ya wasanii walioshiriki shindano hili ikazaliwa. Wasanii waliopendana, kuheshimiana na kushirikiana, wakafarakana sababu ya "Mfalme wa Rhymes 2004".
Profesa Jay, Soggy Doggy, Solo Thang na wakaonesha vinyongo vyao dhahiri kwa Mshjkaji wao Afande kwa ajili ya Ushindi. Wengine wakarejea kumpongeza Dully na kumuona 'ana akili sana' kujiondoa mapema kushiriki.
Wakati baadhi ya wasanii wakidaiwa kusumbuliwa na Jinamizi hilo, Afande yupo zake Morogoro, kijijini kwake "Pori la Simba", akiendelea kucheka tu mpaka jino la mwisho. Kwanini, Kwa sababu "Mfalme wa Rhymes" ni moja tu na hatoweza na kutawazwa mwingine
Hata baada ya msimu wa pili wa "Mfalme wa Rhymes 2005" kujiandaa kufanyika, wasanii wengi walipiga marufuki majina yao kuwekwa, na hivyo shindano hilo kufa rasmi na kubaki kuwa historia ya mapitio ya muziki wa Rap nchini.
Tangu nyakati hizo mpaka leo, "Mfalme wa Rhymes" ameendelea kuwa mmoja tu, kwa sababu mashindano yaliyomfanya kutawazwa yalifanywa mara moja na sidhami kama yatathubutu kufanywa tena.
Julai 27 2024, kwenye ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre - JNICC nikiwa Mwana kamati ya Tuzo za iChange Nations International Awards, nilikutana na Afande Sele.
Mengi tuliyoongea kuhusu Mfalme wa Rhymes 2004 na harakati nyingine nyingi za kijamii na muziki nitayaandika kadiri nitakavyojaaliwa muda na uhai (Inshaallah).
Niwasihi tu wanangu mnaoendelea 'kukunja' mpaka leo, kunjueni tu. Yanini kuongeza makunyanzi moyoni, wakati jamaa hana time, anacheka tu kijijini kwake mpaka jino la mwisho ? Amani iendelee
Mengine yabaki kama historia.
#Balozi..........✍️