Web

Utekaji wa Kiongozi Chadema Wazua Taaruki, Atekwa, Ateswa na Kutupwa Porini



Katika tukio la kusikitisha lililotikisa taifa, Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Aisha Machano, alitekwa nyara mchana kweupe na watu wasiojulikana, akapigwa kikatili, na kisha kutupwa katika pori lisilojulikana.


Tukio hili linaibua maswali mengi kuhusu usalama wa viongozi wa kisiasa na haki za binadamu nchini.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti la Nipashe, Aisha alikuwa akitekeleza majukumu ya kichama wilayani Kibiti, mkoani Pwani, akihamasisha wananchi kujitokeza kugombea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Akiwa katika kituo cha daladala cha Bungu, alikutana na mwanamke aliyedhani ni abiria mwenzake. Walipanda basi pamoja na walipofika kituo cha Jaribu, walishuka wote.

Ghafla, gari aina ya Landcruiser lilifika na wanaume sita waliodai kuwa ni polisi walimkamata kwa nguvu, wakamfunga pingu na kitambaa cheusi usoni, na kisha kuanza safari isiyojulikana.

Walipofika katika msitu, walimshusha na kumfunga kwenye mti, kisha wakaanza kumpiga kwa magongo sehemu mbalimbali za mwili, wakimtuhumu kuwa alitumwa kuchoma vitenge vyenye picha ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Aisha alikanusha madai hayo, akieleza kuwa ilikuwa ni uamuzi wa viongozi wa BAWACHA kuchoma vitenge hivyo kama ishara ya kutoridhishwa na mambo kadhaa, ikiwemo kupotea kwa vijana watano wa chama hicho.

Majibu yake hayakuwaridhisha watekaji, waliendelea kumpiga na kumtishia maisha, wakimtaka ataje viongozi wa CHADEMA waliohusika katika tukio hilo.

Baada ya kipigo cha muda mrefu, watekaji walimvua nguo zote na kumpiga picha za utupu, wakimtishia kuwa wangesambaza picha hizo endapo angezungumza na vyombo vya habari kuhusu yaliyomkuta.

Kisha walimtelekeza katika eneo lisilojulikana. Aisha alitembea kwa muda hadi alipofika kwenye kibanda cha kuuza chipsi na madereva wa bodaboda, ambapo alipoteza fahamu.

Alipozinduka, alijikuta yuko katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mwananyamala, Dar es Salaam, baada ya kuokolewa na bodaboda waliomkuta wilayani Kisarawe.

Jeshi la Polisi lilithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na lilianza uchunguzi kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, DCP David Misime, alitoa wito kwa wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea ili kupata majibu sahihi kuhusu kilichotokea, sababu zake, wahusika, na hatua zitakazochukuliwa kulingana na ushahidi utakaopatikana.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad