Mshtakiwa Shabani Adam ( katikati) na mwanae Mussa Shabani, wanaodaiwa kusafirisha gramu 41.49 za heroine, wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yao kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne.
Dar es Salaam. Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa imeanza vikao vya majadiliano na wanandoa wanaokabiliwa na kesi ya kusafirisha gramu 41.49 za heroni kwa ajili ya kuimaliza kesi hiyo.
Wanandoa hao, Shabani Adamu na mke wake Husna Issa pamoja na mtoto wao wa kiume, Mussa Shabani, wote wakazi wa Manzese na wakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa hizo kinyume cha sheria.
Februari 18, 2025 mahakama hiyo iliruhusu wanandoa hao kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa mashtaka nchini( DPP) ya kuimaliza kesi yao, baada ya kumwandikia barua ya kukiri mashtaka yao na kuomba kupunguziwa adhabu.
Hata hivyo, leo Machi 28, 2025 Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele ametoa taarifa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, kuwa wameanza vikao vya majadiliano.
"Tunaendelea na utaratibu wa majadiliano (Plea Bargaining) na kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na leo tutakaa kikao cha kwanza na kama tutakubaliana basi tutakuja kusaini mkataba mbele ya Mahakama yako," amedai wakili Mwakamele.
Mwakamele alidai kutokana na hali hiyo, wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa baada ya kumaliza kikao cha kwanza, baina ya washtakiwa na jopo la mawakili wanaoendesha majadiliano hayo.
Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 10, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kuendelea na vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi na washtakiwa wamerudishwa rumande.
Washtakiwa hao walimuandikia barua DPP ya kufanya majadiliano, baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na upande wa mashtaka kuwasomea hoja za awali na idadi ya mashahidi pamoja na vielelezo.
Haya hivyo, kiwango hicho wanachodaiwa kukutwa nacho washtakiwa hao kinaruhusiwa kunawaruhusu washtakiwa kufanya majadiliano na DPP.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 11, 2024 eneo la Manzese ambapo wanadaiwa kukutwa na gramu 41.49 za heroini, kinyume cha sheria.