Watu wawili wamepoteza maisha katika matukio mawili tofauti Mkoani Morogoro ambapo mmoja kwa kujinyonga huku mwingine akifariki wakati akiwa anasubiri usafiri wa basi katika kituo kikuu cha mabasi mkoani humo.
Taarifa ya leo Machi 02, 2025 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro, SACP Alex Mkama imeeleza kuwa tukio la kwanza limemhusisha Nungu Nassoro (25), mfanyabiashara na mkazi wa kata ya Lukobe, wilaya na Mkoa wa Morogoro ambaye amekutwa akiwa amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani kwenye mti wa mwembe uliopo kwenye makazi yake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo tukio la Nungu kujinyonga limebainika mapema Machi 01, 2025 katika mtaa na kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro huku uchunguzi wa awali ukibaini kuwa chanzo kujiondoa uhai ni msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa maisha ambapo Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu baada ya kukamilisha uchunguzi wa maiti hiyo.
Tukio lingine limetokea usiku wa kuamkia Machi 2, 2025 katika stendi kuu ya mabasi maarufu kwa jina la Msamvu, Wilaya ya Morogoro ambapo Magnos Simon Timoth Mkinga (22), mwanachuo wa Chuo Kikuu cha Jordan, mwaka wa kwanza, mkazi wa Kipera, Mkoani Morogoro alizidiwa ghafla na kujilaza chini mbele ya dada yake aitwaye Anna Osward Mbonde (42), Mkazi wa Kibaha wakati wanasubiri usafiri wa basi la Kampuni ya Super Feo kwenda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kwaajili ya matibabu.
Juhudi za kumfikisha hospitali zilifanywa na gari ya Polisi iliyokuwa doria, lakini alipofikishwa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro ilibainika kuwa tayari alikwisha fariki huku uchunguzi wa awali ukionyesha kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi, na ndugu zake walikuwa katika mpango wa kutafuta matibabu zaidi ili kuimarisha afya yake. Kwa sasa Maiti imehifadhiwa chumba cha maiti hospitalini hapo kusubiri taratibu za mazishi.