Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, Dk Dorothy Gwajima amewasihi wanaozungumza vibaya kuhusu wanawake waolea watoto wao wenyewe maarufu kama 'Single Mothers' kuacha tabia hiyo kwani hao ni wazazi kama wengine hivyo wanahitaji kuheshimiwa.
Gwajima ameyasema hayo jana Alhamisi jijini Dar es Salaam katika hafla iliyoandaliwa na Taasisi ya Her Initiative na kukutanisha wadau mbalimbali kuzungumzia masuala ya wanawake na uongozi.
Gwajima amesema kutoa kauli mbaya dhidi yao ni kuwanyanyasa wanawake ambao wameamua kusimama na kulea watoto wao wenyewe kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufiwa au kutokea migogoro kati yake na mwenza wake.
"Anayehamasisha hayo hana maadili na wala hajui ukuu wa mama katika dunia, cha kushangaza baadhi ya watu katika jamii wanashabikia lazima tujitafakari," amesema.
Hivyo amesema ajenda ya 'single mothers' hawafai haina tija kwani wapo kati yao ambao ni mifano ya kuigwa katika malezi ya watoto.