Web

Waziri: Tanzania Haina Tena, Marburg, Tumeidhiti.......

Waziri: Tanzania Haina Tena, Marburg, Tumeidhiti.......


Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema Tanzania imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa mlipuko wa Marburg na ameutangazia Umma wa Watanzania kuwa ugonjwa huo umeisha kutokana na kutokuwepo kwa Mgonjwa mwingine yeyote tangu mgonjwa wa mwisho alipopatikana January 28, 2025 na hadi kufikia March 11, 2025 siku 42 zimepita.

Waziri Mhagama amesema hayo leo March 13, 2025 wakati akiongea na Waandishi wa Habari Wilayani Biharamulo, Kagera ambapo amesema siku 42 zimepita tangu mgonjwa wa mwisho alipofariki na kisayansi Tanzania inakidhi vigezo vya kutangaza kuwa mlipuko huo umeisha.

“Tarehe 20 January, 2025, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliutangazia umma na jamii ya Kimataifa juu ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg uliotokea katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, naomba nichukue fursa hii leo tarehe 13 Machi, 2025 kuutangazia umma na jamii ya Kimataifa kuwa, sasa Tanzania haina mlipuko wa ugonjwa wa Marburg”

“Ugonjwa wa “Marburg” ni miongoni mwa magonjwa hatari yanayotokana na virusi ambavyo husababisha kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili na husambaa kwa haraka kwa kupitia kugusa majimaji ya mwili wa mtu au mnyama aliyeathirika na ugonjwa huo ambao husababisha madhara mbalimbali ikiwemo ulemavu na vifo”

Waziri Mhagama amewakumbusha Watanzania kuchukua tahadhari kwakuwa nchi zinazotuzunguka zinaendelea kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Mpox na Ebola, hivyo Tanzania pia ipo kwenye hatari kutokana na mwingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi, pamoja na uwepo wa mipaka ya moja kwa moja baina ya nchi hizi.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad