CAS wametoa majibu yao juu ya sakata hili ambapo wametoa siku 10 pekee kwa klabu ya Simba Sc, bodi ya ligi na TFF kupeleka utetezi wao juu ya rufaa iliyopelekwa klabu ya Yanga Sc ambayo imeonyesha wazi kuwalalamikia Simba Sc, bodi ya ligi na TFF juu ya sakata la kuahirishwa kwa mchezo wa dabi ya kariakoo.
Ahmed Ally kupitia kwenye ukurasa wake wa Instagram amechapisha taarifa fupi inayoeleza kwamba "ondoeni shaka wanasimba, Hii tunavuka".
Ujumbe huu kutoka kwa Ahmed Ally umetafsiriwa kwamba afisa habari wa klabu hiyo amedhamiria kuwatoa wasiwasi mashabiki, wadau na wanachama wa klabu ya Simba Sc juu ya mchezo wao ujao wa hatua ya robo fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika ambao watacheza dhidi ya klabu ya Al Masry uko nchini Misri.
Ikumbukwe kwamba siku chache zilizopita klabu ya Simba Sc kupitia kwa afisa habari wa klabu hiyo Ahmed Ally walitoa "slogan" yao ambayo ni "Hii Tunavuka", kwa lengo la kuongeza morali kwa mashabiki na wachezaji wa klabu hiyo ambao watakuwa na kibarua kizito cha kumenyana na Al Masry kwenye michezo miwili ya hatua ya robo fainali ya michuano hii msimu huu.
Mashabiki na wadau wa klabu ya Simba Sc kwa kiasi kikubwa walikuwa wanasubiri kwa hamu kuona viongozi wao watajibu nini mara baada ya taarifa hiyo kutoka CAS lakini Ahmed Ally amekuja na taarifa ambayo imewaacha na maswali magumu mashabiki na wadau wa klabu hiyo.
Simba Sc wamekuwa na utaratibu wao kutoa taarifa kwa umma kupitia kwenye tovuti na vyanzo vyao vya habari vya klabu yao, mashabiki na wadau wa klabu hiyo wanatakiwa kuendelea kuwa wavumilivu kwa wakati huu wakiwa wanaendelea kusubiri taarifa rasmi ambayo itatolewa na klabu hiyo.
Chanzo: ukurasa wa Instagram wa Ahmed Ally.