Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Tundu Lissu, ametangaza kumvua wadhifa Bi. Catherine Ruge aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho na mtaalamu wa masuala ya jinsia makao makuu ya Chadema, kuanzia leo Jumamosi, Aprili 5, 2025.
Taarifa hiyo imethibitishwa rasmi na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Bi. Brenda Rupia, kupitia mitandao ya kijamii, ikiwa ni siku moja tu baada ya kuibuka kwa waraka kutoka kwa kundi lijulikanalo kama G55, ambalo Ruge anatajwa kuwa miongoni mwa wanachama wake. Kundi hilo linajumuisha pia baadhi ya waliowahi kuwania ubunge katika chaguzi za 2020 na 2025.
Kupitia waraka huo, wanachama wa G55 waliweka wazi msimamo wao wa kupinga uamuzi wa chama kutoshiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao, hatua ambayo inakinzana na msimamo rasmi wa Chadema wa "No Reforms, No Election", unaotaka mabadiliko ya kisheria na kimfumo kabla ya kushiriki uchaguzi. Bi. Ruge, ambaye hapo awali aliwahi kuwa Katibu wa Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), anajiunga na Ndugu Julius Mwita aliyepoteza nafasi yake ya Ukurugenzi wa Sekretarieti mapema wiki hii, kutokana na misimamo inayotofautiana na sera za chama.
Katika waraka waliomwandikia Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, Ruge na wenzake walieleza kuwa kususia uchaguzi hakuwezi kuzuia kufanyika kwake, bali kunaweza kuwa chanzo cha matatizo zaidi kwa chama na viongozi wake kisheria. Walibainisha kuwa kushiriki uchaguzi huku wakihamasisha wananchi kudai haki ni njia bora zaidi ya kupambana na hujuma.
“Mazoea ya kutaka kuzuia uchaguzi pasipo ushiriki ni sawa na kujihusisha na jinai. Njia sahihi ya kuzuia uchaguzi usio wa haki ni kwa chama kushiriki na kutumia wagombea wake kuongoza harakati za kupinga ukiukwaji wa haki vituoni,” wamesema katika waraka huo. Kundi hilo pia limekosoa vikali mpango wa Chadema wa kususia uchaguzi, likisema hauna msingi wa kikatiba na unakiuka haki za wanachama waliotaka kugombea uongozi kupitia chama hicho, kama inavyoruhusiwa na ibara ya 5.2.2 ya Katiba ya Chadema.
Miongoni mwa waliounga mkono hoja hizo ni pamoja na vigogo wa chama kama Mawakili John Mallya, John Mrema na Julius Mwita, waliotahadharisha kuwa hatua hiyo ya kususia uchaguzi inaweza kutafsiriwa na wadau wa demokrasia kuwa ni ishara ya uasi. “Wadau wengi wa demokrasia nchini wanaafiki hoja ya kudai mabadiliko (reforms), lakini wanaona mpango wa kususia uchaguzi kama kitendo kinachoenda kinyume na misingi ya kikatiba na sheria za nchi,” imesema sehemu ya waraka huo. Jitihada za JamboTv kumpata Bi. Catherine Ruge kwa ajili ya maoni zaidi bado zinaendelea, baada ya juhudi za awali za kuwasiliana naye kutokufanikiwa.
From Opera News