Chukua Hii Mtu Wangu, Kumbe ni KOSA la Jinai Kupekua Simu ya Mpenzi Wako
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania kitengo cha Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto Makao Makuu ya Polisi Dar es salaam, Afande Wilfred Willa amewakumbusha Watanzania kuwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kosa la jinai kupekua simu ya Mpenzi au ya Mtu bila ridhaa yake.
Akizungumza baada ya kutoa semina kwa Makundi maalumu likiwemo kundi la Polisi Jamii na Makundi mbalimbali Mkoani Geita, Afande Willa amesema amelazimika kuyakumbusha hayo kwakuwa kumekuwa na changamoto kubwa sana katika Familia hasa kwa Mke na Mume kugombania simu kwa nia ya kutaka kupekua kutazama kilichomo.
“Unakuta Mwanamke au Mke anagombania simu ya Mume wake na Mume anagombania simu ya Mke wake sio kwa nia njema ila kwa nia ovu kwa lengo la kupekua simu ya mwenzie, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila Mtu ana haki ya faragha na usiri wa taarifa zake na mambo yake anayoyafanya yeye kama yeye anafaragha kwahiyo ukifanya hivyo bila ridhaa yake unakuwa umeingilia faragha yake na kufanya kuwa kosa la Jinai” Afande Willa