"Tunaposema G- 55 siyo kwamba tupo 55, 55 imetumika tu kama alama ya kuwakilisha kundi, kundi hili liliundwa baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA kualika wagombea wa mwaka 2020 wa ubunge na waliotia nia mwaka huu kwenye kikao cha tarehe 3 Aprili Makao Makuu ya chama (CHADEMA). Sisi kama wagombea na ambao hatuna sehemu ya kukutana, tukaunda kundi sogozi la WhatsApp ili kuweka mawazo yetu kwa pamoja na hatimaye tuweze kuyawakilisha kwa Katibu Mkuu. Kwahiyo lilikuwa ni kundi ambalo tunajaribu kuweka mawazo, maoni, tunashauriana kwa pamoja kama yalivyo makundi mengine mbalimbali ndani ya chama, kwenye chama chetu kuna makundi kwenye kata, vitongoji na tungeweza hata kuliita CHADEMA Family, kwasababu makundi hayo yapo kila mahali kwenye chama chetu, kwahiyo ndivyo ambavyo kundi letu la G- 55 lilivyoundwa. Kundi hili lina wajumbe wengi na bado tunaendelea kushauriana mambo mbalimbali ya chama na mikakati yetu binafsi kama wagombea tunawezaje kupata rasimali, tunawezaje kujipanga na kampeni, na tunapeana uzoefu"- Mrema.
John Mrema, mmoja wa wanaounda kundi la G-55 ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akizungumza na wanahabari mkoani Dar es Salaam siku ya Jumapili Aprili 6, 2025.