![]() |
Klabu ya Simba Sc imetangaza rasmi viingilio kwa ajili mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) utakaopigwa Aprili 20, 2025 katika dimba la New Amaan Complex, Zanzibar majira ya saa 10:00 jioni.
Akizungumzia mchezo huo kwenye mkutano na waandishi wa Habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally amesema viingilio vya mchezo huo ambao umepewa Kaulimbiu ya HATUISHII HAPA ni VIP A - Tsh. 40,000, VIP B - Tsh. 20,000 na Mzunguko ni Tsh. 10,000 huku akibainisha kuwa tiketi zitauzwa kwa mfumo wa N-Card.
“Uwanja wa Amaan unaingiza watu 15,885. Viingilio ni VIP A - Tsh. 40,000, VIP B - Tsh. 20,000 na Mzunguko ni Tsh. 10,000. Tiketi zitauzwa kwa mfumo wa N-Card. Kuanzia hivi sasa tiketi zinapatikana katika maeneo mbalimbali. Kwa wale wa Dar es Salaam vituo vyote ambavyo vinauza tiketi vitaendelea kuuza tiketi kama kawaida.”——amesema Ahmed Ally
“Kwa ndugu zangu wa Zanzibar ambao wamezoea kununua tiketi za karatasi kwasasa wanaweza kununua tiketi za N-Card na ukawa nayo hadi siku ya mchezo. Siku ya mchezo tiketi hazitauzwa nje ya uwanja na maeneo mengine yataendelea. Utaratibu huu ni wa CAF. Yeyote ambaye anahitaji tiketi anunue tiketi sasa.”
“Hii Simba inayokuja kucheza Zanzibar ni mpya kabisa, Watu wa Dar wao wameshaiona kwenye mchezo wa robo fainali. Sizungumzii kuangalia kwenye TV, kuangalia live. Simba ya nusu fainali ni nyingine kabisa, mnaenda kushuhudia kila kitu kipya. Hii sio mechi ya mtu kuangalia kwenye tv, sio mechi ya kuhadithiwa, hii ni mechi ya kuangalia kwa macho ya nyama. Hii ni mara ya kwanza Simba ikiwa katika nafasi ya nne kwa ubora Afrika kucheza.”——amesema Ahmed Ally