Suala la kuhalalishwa na kupunguziwa makali kwa pombe ya kienyeji aina ya Gongo ili kutumika kama chanzo cha kipato kwa wananchi, limeendelea kuibuliwa na Wabunge ambao wanaitaka Serikali kuangalia namna ya kuchakata pombe hiyo kwa viwango salama vya matumizi.
Leo Aprili 15, 2025 bungeni jijini Dodoma, Mbunge wa Jimbo la Momba, Mhe. Condester Sichalwe, ameuliza Wizara ya Viwanda na Biashara kuhusu idadi ya mitambo iliyosambazwa kwa wananchi wanaojihusisha na uzalishaji wa pombe ya Gongo.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Wizara hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema pombe ya Gongo ni kinywaji chenye kilevi kikubwa ambacho hutengenezwa kienyeji, na kwa sasa Serikali haijahalalisha uzalishaji wake rasmi kutokana na madhara yake kwa afya ya binadamu.
“Kwa msingi huo, mpaka sasa hakuna mitambo ya kutengeneza pombe ya Gongo iliyosambazwa kwa wananchi, na Serikali haijaanzisha mpango wowote wa kufanya hivyo,” amesema Dkt. Kiruswa.
Katika swali lake la nyongeza, Mhe. Sichalwe alitaka kujua kwa nini Serikali inashindwa kuboresha pombe hiyo ya kienyeji na badala yake kuruhusu uingizwaji wa pombe kali kutoka nje, ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiharibu afya na mustakabali wa vijana nchini.