Mbunge wa Geita Vijijini, Mhe. Joseph Musukuma, amesema kuwa kampeni ya No Reform No Election inayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) haina nafasi ya kufanikiwa kwa sababu haina uwezo wa kuzuia uchaguzi mkuu. Aidha, amedai kuwa kuna mipango inayoendelea ndani ya chama hicho ya kutaka kumwondoa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Musukuma amesema kuwa siasa siyo kususia uchaguzi bali ni kushiriki kwa ushindani, na madai ya kususia uchaguzi yanatokana na hofu ya kushindwa.
"Bila wao, sioni kama kuna raha. Watu wanasubiri tu hiyo kauli ya No Reform No Election, lakini ndani ya CHADEMA kuna jambo kubwa zaidi ya 'No Election'. Tuendelee kuwa hapa tu, natamani mwezi ujao tuone yatakavyokuwa. Hii G-55 si watu wajinga; kama ni chama chenye demokrasia, Mwenyekiti alipaswa kusitisha ziara na kuwasikiliza wanachama wake, si kuwaita wajinga,
Unatangaza kuzuia uchaguzi bila kueleza mbinu. Kama kuna Rais ambaye amewapa uhuru mkubwa wana-CHADEMA, ni Rais Samia Suluhu Hassan. Nimekuwepo wakati wa Kikwete na Magufuli, hawakuwa na uhuru huu. Sasa mnapopewa uhuru, mnaanza kuweka masharti. Sisi tayari tumejiandaa kwa uchaguzi." Amesema Musukuma.