Kuwalaumu Azam FC kwa nini walipoteza Mchezo ni Kuwakosea Heshima Singida Black Stars
Baada ya Azam FC kupoteza mchezo jana kwa kufungwa goli 1-0 na Singida Black Stars pale uwanja wa Liti, Singida, nimeona maandiko na mijadala mingi kupitia vyombo mbalimbali vya habari wakilaumu imekuaje Azam imefungwa na Singida Black Stars!
Wengine wakafika mbali zaidi na kusema pengine huenda wachezaji hawakujituma wakitunza nguvu kuusubiri mchezo wao ujao dhidi ya Yanga [April 10, 2025] pale Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwanza kuwalaumu Azam FC kwa nini walipoteza ule mchezo ni kuwakosea heshima Singida Black Stars, kwamba hawakustahili kushinda mbele ya Azam FC kitu ambacho si sawa. Singida Black Stars imesheheni wachezaji wengi wenye madaraja ya juu hata nafasi waliyopo kwenye msimamo wa ligi [4] hawapo kwa bahati mbaya.
Tukirejea kwa Azam FC, kufungwa 1-0 na Singida Black Star inawezekana kuna sababu nyingi za kiufundi na kimbinu ndani ya uwanja. Mimi naangazia sababu moja kubwa ya nje ya uwanja ambayo huenda imepelekea kwa kiasi kikubwa Azam kupoteza siku ya jana.
Aprili 3, 2025 Azam FC ilicheza mchezo wa Ligi jijini Mbeya [KenGold 0-2 Azam FC] baada ya mchezo wa Mbeya, wakalazimika kusafiri kwenda Mkoani Singida kucheza na Singida Black Stars Aprili 6, 2025.
No muda wa kupumzika wachezaji wanatakiwa kusafari [Mbeya-Singida], kumbuka hakuna safari ya ndege ya Mbeya-Singida! Uwanja wa ndege wa karibu na Singida ni Dodoma, kwa bahati mbaya hakuna safari ya ndege ya Mbeya-Dodoma!
Kwa hiyo wachezaji wa Azam FC walisafiri umbali mrefu kwa njia ya barabara na kuzalisha uchovu, hivi vitu lazima pia tuviangalie kwa sababu wanaocheza pia ni binadamu na sayansi inawataka kupumzika walau saa 72 baada ya mchezo mmoja hadi mwingine.
Kabla ya kuwahukumu Azam FC kwa kupoteza mchezo sai uliopita dhidi ya Singida Black Stars tuangalie na kujiridhisha kila kitu kilikuwa sawa?