Rushwa michezoni, ni miongoni mwa mambo yaliyopewa katazo na kuwekewa adhabu kali sana ulimwenguni kote, hiyo inaenda sambamba na uwepo wa matendo ya udanganyifu na upangaji wa matokeo, matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo nk, vyote hivyo ni miongoni mwa mambo yaliyopigwa marufuku karibu na mashirikisho ya michezo yote Duniani
Kwa upande wa mpira wa miguu kama ilivyokuwa kwa michezo mingine, na ikizingatiwa kuwa huo ni mchezo pendwa namba moja Duniani sheria imekuwa kali sana, hapa mamlaka za soka ulimwengu zikiongozwa na Shirikisho la soka Duniani (FIFA) limeenda mbali zaidi kwa kueweka sheria na adhabu kali sana kwa serikali zitakazoingilia maamuzi ya mpira wa miguu
Hapa ieleweke wazi kuwa, haijapigwa marufuku serikali kusaidia au kushiriki kwenye shughuli za michezo hususani mpira wa miguu la hasha, ila kilichopigwa marufuku ni serikali kujiingiza kwenye kufanya maamuzi ya masuala ya soka, adhabu ya jambo hilo endapo ikibainika ni pamoja na Taifa husika kufungwa kujihusisha na masuala ya Soka, kama ilivyo kwa nchi ya Congo kwa sasa
Ndio maana sio dhambi kwa serikali kulipa mishahara, posho nk kwa wachezaji au makocha wa klabu au timu za Taifa kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kusaidia ukuaji wa michezo kwenye nchi husika, na ni ukweli usiopingika kuwa ni ngumu kwa vyama vya michezo kuendesha shughuli zake bila kuwa na ushirikiano thabiti na mamlaka za kiserikali, hata hivyo endapo ikatokea kuna mashauri na sintofahamu imejitokeza kwenye mpira wa miguu kwa mfano na inahitajika kufanyiwa maamuzi basi hapo umewekwa utaratibu mahsusi kuanzia ngazi za chini hadi FIFA, na katu katika hilo imepigwa marufuku 'mpira kupelekwa Mahakamani'
Pamoja na yote hayo, lakini inapotokea masuala ya Rushwa au viashiria vyake, basi moja kwa moja licha ya kwamba mamlaka za mpira zinaweza kuchukua hatua zake lakini pia si dhambi kwa vyombo vya kiserikali, na kwamba Tanzania mfano TAKUKURU au ZAECA kuingilia kati na kushughulika na wale wanaohisiwa kujihusisha kupokea au kutoa rushwa kwa namna moja au nyingine