Mwanadada mashuhuri Carolina Hawa, maarufu kama Carina, amefariki dunia leo huku akiwa katika maandalizi ya kurejea nyumbani kutoka India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana hivi punde, Carina alikuwa amefanyiwa upasuaji mkubwa kwa ajili ya kutibu tatizo la tumbo lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu. Inasemekana hali yake ilikuwa ikielekea kuimarika, na alitarajiwa kurejea Tanzania leo.
Vyanzo vya karibu na familia vinaeleza kuwa taarifa rasmi kutoka kwa jamaa wa karibu na madaktari waliomhudumia zinatarajiwa kutolewa hivi karibuni.
Carina alijipatia umaarufu kupitia shughuli mbalimbali za kijamii na mitandao ya kijamii, ambako aliweka wazi changamoto zake za kiafya, hatua iliyowagusa wengi na kuibua wimbi la maombi na michango kutoka kwa watanzania wa ndani na nje ya nchi.
Mpaka sasa, wapenzi, ndugu na marafiki wameendelea kueleza masikitiko yao kupitia mitandao ya kijamii, wakimtaja Carina kama mtu aliyekuwa na moyo wa kupambana na matumaini licha ya maumivu aliyokuwa akiyapitia.