Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika TLS,Wakili Boniface Mwabukusi ameeleza kusikitishwa na tafsiri ya sheria inayochukuliwa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, akisema hakuna sheria inayozuia Chama cha siasa kushiriki uchaguzi kwa kutosaini Kanuni za maadili ya uchaguzi.
Kupitia ukurasa wake wa X Mwabukusi ameandika kusema;
"Sijui hawa wenzetu wanazisomaje hizi sheria, Je ni utofauti wa vyuo? Hakuna sheria inayozuia chama kushiriki uchaguzi kwa kutosaini maadili ya uchaguzi ni tafsiri mbovu ya kukosa logic (maana). Tuache kuharibu Taifa na kuchochea vurugu." ameandika Wakili Mwabukusi.
Mtazamo wa Mwabukusi unashabihiana na mtazamo wa Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu ambaye jana Jumamosi amependekeza kwamba chama ambacho hakitasaini kanuni za maadili ya uchaguzi kisizuiwe kushiriki uchaguzi Mkuu kwa kuwa ni haki ya Kikatiba.
“ACT-Wazalendo tuliwasilisha maoni kwamba haki ya chama cha siasa kushiriki uchaguzi ni ya kikatiba, kusaini (kanuni za maadili) kuwe ni ‘commitment’ tu peke yake na siyo kukiondolea chama haki ya kushiriki katika uchaguzi” alisema Ado Shaibu.
Jana Aprili 12, Vyama 18 vyenye usajili wa kudumu nchini Tanzania vilisaini kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu na kulingana na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhan Kailima, @ChademaTz haikufika kusaini kanuni hizo suala ambalo limeelezwa kuwa kutokana na kutosaini kwao wamepoteza sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo zitakazofanyika ndani ya miaka mitano 2025/30.