Web

Mwanzo au Mwisho wa G-55 Ndani ya Chadema?

 

Mwanzo au Mwisho wa G-55 Ndani ya Chadema?

Miaka 32 iliyopita katika siasa za Tanzania kuliibuka kundi la wabunge 55 waliojiita G-55 ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), lililotaka mabadiliko ndani ya chama ya kuleta Serikali ya Tanganyika ndani ya Tanzania. Lilitikisa sana utawala wa Rais wa wakati huo, Ally Hassan Mwinyi na lilionekana kama kundi la waasi.


Kama si kuingilia kati kwa viongozi wakuu akiwemo Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, leo pengine kungekuwa na mpasuko zaidi ndani ya chama na kubadili siasa za nchi kwa miaka mingi. Harakati za kundi hilo, zimesalia kuwa historia kubwa Tanzania.


Miaka 32 baadae miezi michache kabla ya uchaguzi Mkuu na Katikati ya vuguvugu la No Reforms, No election liliibuka kundi lingine G-55 ndani ya CHADEMA, linaloupinga wazi Msimamo wa No Reform, No Election.


'Wanaotaka uchaguzi ni wengi kuliko wanaotaka kuzuia uchaguzi, kwa sababu hawaoni huo muujiza wa kuzuia uchaguzi', anasema John Mrema, mmoja wa wanachama wa G-55.


No Reforms, No Election, ni msimamo wa kisera wa chama hicho uliopitishwa na Kamati Kuu katika kikao chake cha Disemba 2-3, 2024 chini ya mwenyekiti aliyepita, Freeman Mbowe kabla ya kupata baraka ya Mkutano mkuu wa Januari 21, 2025 ulioongozwa na Mbowe, mkutano ambao pia ulimchagua mwenyekiti mpya, Tundu Lissu.


Kwa kupinga namna ya utekelezaji wa msimamo huo wa chama, kundi la G-55 linaonekana kuwa kundi lingine la 'uasi' ndani ya chama, linaloasi maamuzi yaliyopitishwa na vikao halali vya vyama. Hii ni dhana inayojengwa na dhana nyingine inayohusisha makovu ya uchaguzi uliopita wa ndani wa chama, uchaguzi wa Januari, 2025.


Ulikuwa uchaguzi wenye mvutano mkali kuwahi kutokea kwenye siasa za vyama vingi Tanzania. Lissu akimbwaga kigogo aliyeongoza chama kwa miaka zaidi ya 20, Mbowe katika nafasi ya Uenyekiti kwa kupata kura 513 dhidi ya 482 alizopata Mbowe.

Leo ni kama ukurasa mwingine umefunguliwa, kulingana na Katiba na sheria za uchaguzi, hakuna mgombea anayeruhusiwa kugombea bila kuwa mwanachama wa Chama fulani cha siasa, Pili, hakuna Chama ama mgombea anayeweza kuwania nafasi yoyote ya kiuchaguzi bila ya Chama chake kuwa tayari kimesaini Kanuni za maadili ya Uchaguzi ambazo kiutaratibu zimesainiwa leo Jijini Dodoma yalipo makao makuu ya Tume huru ya Taifa ya uchaguzi.


Kulingana na Taarifa ya Mkurugenzi wa uchaguzi kati ya vyama 19 vilivyo na usajili na sifa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2025, ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema ambacho hakikusaini Kanuni hizo za Maadili ya uchaguzi, Moja kwa moja kikipoteza haki yake ya kushiriki, wanachama wake kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.


Huu ni Mwanzo ama Mwisho wa vuguvugu la G55 lenye kuwawakilisha watia nia ya ubunge wa Chadema kwa mwaka 2020 na wa 2025 zaidi ya 200 sambamba na baadhi ya waandamizi wengine ambao wanatajwa tajwa na G55 bila ya kufunuliwa wazi ama kutajwa kwa wananchi pahala popote " labda huenda ni kwa kuhofia nafasi zao ndani ya Chadema".


Bungeni Mjini Dodoma kunapoendelea vikao vya Bajeti ya mwaka 2025/26, Wiki hii napo kulipamba moto, Waliokuwa wabunge wa Chadema ' Kabla ya kukanwa na kuachwa yatima Bungeni' Wamesimama kidete - Ikiwa ni mkutano wa mwisho kabla ya kuvunjwa kwa Bunge mwezi Julai, Wengi wameapa kurudi Bungeni, wakikosoa maamuzi yaliyochukuliwa ya No Reforms, No Election.


Mbunge pekee wa Jimbo, anayewakilisha wananchi wa Nkasi kupitia Chadema, Aida Kenani alipozungumza na JamboTv wiki hii alikiambia chombo hiki cha habari kuwa suala la yeye kurudi Bunge lijalo anamuachia Mungu na wananchi wa Nkasi wanaojua walipomtoa na kwanini walimpa nafasi ya kuongoza miaka mitano iliyopita, Salome Makamba wa Viti maalum yeye alieleza kuwa yu' tayari kwa uchaguzi, atashiriki na atakuwepo katika Bunge lijalo.


Akikaririwa na Gazeti moja la kila siku nchini, likichapisha habari zake kwa Lugha ya kiswahili, John Mrema, mwanasiasa wa Chadema na kinara miongoni mwa wazungumzaji wakubwa wa G55 ameeleza kuwa wameipata taarifa ya Chadema kutojitokeza kusaini Kanuni za maadili, akieleza kuwa wanajiandaa kuzungumza na umma.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad