Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, ameweka wazi msimamo wake kuhusu hoja zinazoibuliwa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuhusu unyonyaji katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye zao la korosho, akisema wengi wao walikosa ujasiri wa kuwatetea wakulima wakati suala hilo lilipokuwa likipigiwa kelele bungeni mwaka 2018.
Akizungumza mbele ya wakazi wa Kilwa mkoani Lindi siku ya Alhamisi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika wakati wa ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, Nape amesema ni unafiki kwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani kujifanya kuwa na uchungu na zao la korosho wakati historia inaonesha walikaa kimya wakati wakulima walihitaji sauti yao.
Akimtaja aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Godbless Lema, Nape alisema licha ya kuwa na fursa ya kuwatetea wakulima wa korosho wakati wa mjadala mzito bungeni, alichagua kunyamaza.
“Tulikuwa tunapigana kwa ajili ya wakulima wa korosho, tukasimama kuwatetea, lakini hawa walikaa kimya. Leo wanajifanya wana uchungu, ni wanafiki,” amesema Nape.
Katika kueleza mchango wa serikali ya sasa, Nape amesema hakuna Rais aliyewahi kusimama na mkulima wa korosho kama Rais Samia Suluhu Hassan. “Wanakulwa, wanakusini, wakulima wa korosho, nataka niseme hivi, katika historia ya zao la korosho, hakuna Rais aliyesimama na mkulima kama Mama Samia. Hayupo!” amesisitiza