KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.Emmanuel Nchimbi amesema kuwa ni kosa la kisheria na kikatiba kukilazimisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kushiriki uchaguzi bali kiungwe mkono kwenye msimamo wao wa kutoshiriki uchaguzi.
Amesema inapofika wakati wa uchaguzi hakuna raia anayeweza kusema uchaguzi usifanyike hata Rais, Makamu, Waziri Mkuu hawezi kulitamkia Taifa kwasababu ni takwa la kikatiba, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kwa kuwa uchaguzi mkuu wa 2025 utafanyika.
“Nawahakikishia uchaguzu mkuu wa mwaka 2025 utafanyika.Pamoja na haki ya raia kugombea ni kosa kubwa kulazimisha chama chochote kuingia kwenye uchaguzi, kuna taarifa za kuilazimisha CHADEMA kuingia kwenye uchaguzi waacheni ni haki yao kikatiba, kisheria kususia,”amesema.
Aidha, amesema hata kikibaki chama kimoja uchaguzi utafanyika na kwamba kwa ambao hawataki kushiriki waungwe mkono kwa uamuzi wao wa kutoshiriki.
“Nawasisitiza kuna uchaguzi wa 20230 mtu yeyote asiwalazimishe CHADEMA kukaaa kuwasema CHADEMA kila siku ni kinyume cha Katiba na sheria, Lissu (Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa) ana haki kabisa na tutawaunga mkono watakachoamua.
“Tunachowaomba Lissu na wenzake wasipoteze haki zote mbili watumie vizuri ya kuchagua na kuchaguliwa, watumie haki yao ya kuchagua viongozi kwenye uchaguzi ujao, na kwakuwa nasi tunawaunga mkono msimamo wao wa kususia,”amesema.
Aidha, alimuomba Lissu na wenzake ambao hawataki uchaguzi kumpa kura ya ndio kwa wagombea wa CCM watakaoshiriki uchaguzi mkuu, na kwamba haitapendeza wakapoteza haki zote mbili zilizopo kikatiba.