Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amewataka mashabiki wa soka nchini kuwa na subira kuhusu sakata la kutofanyika kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba SC na Yanga SC, maarufu kama Dabi ya Kariakoo.
Waziri Kabudi ameleza leo Aprili 14, 2025 jijini Dodoma kuwa mamlaka husika, ambazo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ndizo zenye mamlaka ya kutoa taarifa rasmi kuhusu hatma ya mchezo huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Kabudi alifafanua kuwa, “Waziri hawezi kuingilia ili kufikia wao kuwa na maridhiano. Nawaomba Watanzania wawe na subira kwa sababu jambo hilo, hizi klabu zinawafuasi na mashabiki katika nchi mbalimbali, hakuna budi kuienzi na kuheshimu ukubwa wa vilabu.”
Mchezo huo, uliopangwa kufanyika Machi 8, 2025, uliahirishwa kutokana na mvutano kati ya klabu hizo mbili. Simba SC ilidai kuwa haikuruhusiwa kufanya mazoezi ya awali uwanjani na hivyo kuamua kutoshiriki mchezo huo, wakati Yanga SC ilisisitiza kuwa mchezo huo ungechezwa kama ulivyopangwa. Baadaye, Bodi ya Ligi iliahirisha rasmi mchezo huo, ikitaja sababu za kiusalama na mazingira ya dharura.
Katika juhudi za kutatua mgogoro huo, Waziri Kabudi alikutana na viongozi wa klabu zote mbili pamoja na TFF na TPLB mnamo Machi 27, 2025. Kikao hicho kililenga kusikiliza pande zote na kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Hata hivyo, hadi sasa, hakuna tamko rasmi lililotolewa kuhusu hatma ya mchezo huo.
Waziri Kabudi alisisitiza kuwa wizara yake haina mamlaka ya kuingilia masuala ya ligi na kwamba ni jukumu la TFF na TPLB kutoa maamuzi na taarifa rasmi. Alitoa wito kwa mashabiki wa soka nchini kuwa na subira wakati mamlaka husika zikishughulikia suala hilo.