Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC Ahmed Ally amesema Mgeni maalum wa mchezo wao wa robo fainali dhidi ya Al Masry ni Mjumbe wa Kamati Utendaji ya CAF, Rais wa CECAFA na Rais wa TFF, Wallace Karia akisema wana kila sababu ya kumpa nafasi hii kwa kutambua mchango wake na kwa kuheshimu mchango wa Wallace Karia kwenye mpira wa Tanzania.
Ahmed amesema hayo leo April 04,2025 Mbezi Shule Sokoni Jijini Dar es salaam ambako kumefanyika hamasa kuelekea mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) dhidi ya Al Masry itakayochezwa Aprili 9, 2025 iliyoambatana na uzinduzi wa kispika cha hii tunavuka.
“Mgeni maalumu wa mchezo wetu wa robo fainali dhidi ya Al Masry ni Mjumbe wa Kamati Utendaji ya CAF, Rais wa CECAFA na Rais wa TFF, Wallace Karia, tuna kila sababu ya kumpa nafasi hii kwa kutambua mchango wake, tunatambua, tunaheshimu mchango wa Wallace Karia kwenye mpira wa Tanzania, Simba SC kufika nafasi ya sita kwa ubora Afrika ni katika uongozi wa wake”
“Jambo la msingi tukiwa uwanjani ni ustaarabu wetu, tunapokwenda uwanjani tujiepushe na aina yoyote ya vurugu, twendeni tukashangilie kwa nguvu tukiingia nusu fainali, mwisho niwahamasishe Wanasimba wenzangu kununua tiketi za mchezo dhidi ya Al Masry”
“Wanatuonea wivu sisi kuwa hapa, sasa niwambie yeyote ambaye atatia mkono kwenye hili aache ameandika wosia kwenye Familia yake, kama wanadhani tunatania basi tutakutana safari hii, hii mechi tunaitaka, na tunaitaka sana, tayari tumeshacheza robo fainali tano, hii ya sita tunataka kwenda nusu fainali, Al Masry watake wasitake tutaenda, safari hii hatuishii robo fainali, tunasema kwa kauli moja HII TUNAVUKA”