Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme nchini Tanzania (TANESCO) imetangaza kusikitishwa na kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, kilichotokea leo Jumapili tarehe 13 Aprili 2025 kufuatia ajali ya gari iliyotoke katika Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara.
Bodi ya Wakurugenzi kupitia taarifa yake iliyotumwa kwa wanahabari na idara ya mawasiliano kwa wateja imeeleza kuwa Bodi inatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wafanyakazi wa TANESCO, na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa.
" Taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi na shughuli nyingine za maombolezo zitatolewa kadri mipango inavyoendelea kuratibiwa." Imesema taarifa ya Bodi ya Tanesco.
Injinia Nyamo-Hanga alikuwa na uzoefu wa kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 katika Sekta ya Nishati nchini Tanzania. Amekuwa akifanya kazi na REA tangu mwaka 2008 wakati Wakala ilipoanza shughuli zake na ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya REA ikiwa ni pamoja na Meneja wa Misaada ya Kiufundi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soko & Technologies na Kaimu Mkurugenzi Mkuu.
Alikuwa na Shahada ya Uhandisi (Umeme – UDSM), Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Uhandisi (UDSM), Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA - UDSM), Stashahada ya Uzamili ya Sheria, Usuluhishi na Uamuzi (Taasisi ya Kazi za Jamii Tanzania) na Shahada ya Fedha (Chuo Kikuu cha Strathclyde Glasgow Uingereza).
Injinia Gissima Nyamo-Hanga alikuwa Mhandisi mtaalamu aliyesajiliwa: P.Eng(T) Namba 4503, mwanachama wa taasisi ya usimamizi wa miradi (PMI – U.S.A.), mwanachama wa jumuiya ya kimataifa ya nishati ya jua (ISES), mwanachama wa taasisi ya usuluhishi Tanzania na mtaalam aliyesajiliwa katika tathmini za athari za mazingira na kijamii kwa miradi ya nishati (NEMC – Tanzania).