Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhan Kailima amesema Vyama 18 vya Siasa vimeridhia kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa mwaka 2025 na hivyo kupata sifa ya kushiriki kwenye uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu sambamba na chaguzi nyingine zote ndogo zitakazofanyika ndani ya miaka mitano ijayo.
Vyama hivyo ni AAFP, ACT WAZALENDO, ADA-TADEA, ADC, CCK, CCM, CHAUMA, CUF, MAKINI, DP, NCCR-Mageuzi, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD na UPDP.
Vyama vya siasa 18 kati ya 19 ndivyo vimesaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi 2025 na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakijasaini.
Akizungumza katika hafla ya kusaini kanuni za maadili, Kailima ameeleza wajibu wa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi kwa mujibu wa kifungu namba 162(2) cha sheria hiyo pamoja na aya ya 1.2 ya kanuni za maadii ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, kanuni zinapaswa kusainiwa na wahusika kwa kila chama cha siasa, serikali na Tume.
“Maadili ya uchaguzi ni muhimu katika kuwezesha uchaguzi huru na haki ni muhimu kwa pande zote kuhusika na kusaini maadili hayo, mchakato wa maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani hushirikisha wadau na tunawashukuru wadau wote kwa maoni mliyotoa wakati wa maandalizi ya kanuni hizi," alisema.
Kulingana na Gazeti la Nipashe, Mkurugenzi wa zamani wa Itifaki, Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, John Mrema alipoulizwa kuhusu ushiriki wao katika mchakato wa uchaguzi ikiwa chama chao hakijatia saini kanuni hizo za maadili hivi leo amesema watakuna ili kutoa tamko lao na namna watakavyofanya.