Mtoto Nilsa Mnyola, aliyegusa mioyo ya Watanzania wengi kupitia mitandao ya kijamii kutokana na hali yake ya kiafya, ameaga dunia usiku wa kuamkia leo.
Nilsa, aliyekuwa akisumbuliwa na tatizo la kichwa kikubwa (Hydrocephalus), alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, baada ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kugharamia matibabu yake.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Simon Mnyola (@jayone_tl), ameelezea kwa uchungu mkubwa safari ngumu ya maisha ya mwanae, akisema Nilsa alizaliwa kabla ya wakati (njiti) na tangu kuzaliwa alionekana kuwa na tofauti ya mwonekano wa kichwa ikilinganishwa na watoto wengine.
Akizungumza na @saditz_official, Simon Mnyola amesimulia mapambano, matumaini na juhudi zilizofanyika kuokoa maisha ya mwanae, safari ambayo iligusa hisia za watu wengi ndani na nje ya nchi.
Mwili wa marehemu Nilsa Mnyola utaagwa katika Kanisa Katoliki Muhimbili, tarehe 20, 2026, kabla ya taratibu nyingine za mazishi.
Jamii imeendelea kutoa salamu za rambirambi kwa familia ya Mnyola, ikiungana nao katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
