BEKI wa zamani wa Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, Ismael Olivier Toure, amejiunga na kikosi cha Simba kupitia kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Huyo anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Wekundu wa Msimbazi kipindi hiki baada ya Libase Gueye wa Senegal na Nickson Kibabage.
Awali, zilikuwa ni tetesi tu lakini leo Januari 20, 206, klabu ya Simba imemtambulisha rasmi kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Mlinzi wa kati huyo mwenye umri wa miaka 28, ametua Msimbazi akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na FC Baniyas ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) tangu Oktoba, 2025.
Ikumbukwe, alijiunga na klabu hiyo msimu wa 2024-25 lakini aliishia kucheza mechi saba pekee, kabla ya kuacha nayo.
Hii inakuwa mara ya pili kwa Toure kufanya kazi na kocha wa sasa wa Simba, Steve Barker, kwani walikuwa wote Stellenbosch.
Kabla ya mabosi wa Simba kuinasa saini yake, Toure alikuwa kwenye rada za vigogo wa Afrika Kusini, Kaizer Chiefs.
