Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni ya Marekani, Jim Risch, amekataa msamaha wa umma uliotolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, akisema haukuwa wa maana wala wa kujitosheleza.
Katika taarifa ya Ijumaa, Januari 30, Risch alisema Muhoozi, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, alivuka mstari mwekundu licha ya kufuta ujumbe wake mtandaoni, na kuongeza kuwa; Marekani itatathmini upya ushirikiano wake wa kiusalama, unaojumuisha vikwazo na ushirikiano wa kijeshi na Uganda.
Kupitia mtandao wa X (Twitter), Kainerugaba aliutuhumu Ubalozi wa Marekani nchini Uganda kwa kumsaidia kiongozi wa upinzani, Kyagulanyi (#BobiWine) kutoroka wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika usiku wa Januari 16, 2026. Hata hivyo, baadaye alifuta ujumbe huo na kuomba radhi, akieleza kuwa alichapisha taarifa hizo kutokana na kupotoshwa na taarifa zisizo sahihi.
