
Ligi Kuu ya Marekani, Major League Soccer, imemtangaza mchezaji wa Ghana Yaw Yeboah kufungiwa maisha kushiriki mashindano ya ligi hiyo baada ya uchunguzi kubaini kuwa alihusika na kamari kwenye mechi za soka.
Uamuzi huo ulitangazwa Jumatatu (Machi 9, 2026) baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa kufuatia taarifa za miamala ya kamari yenye mashaka zilizobainika kupitia washirika wa uadilifu wa ligi. Uchunguzi huo ulibaini kuwa Yeboah na mchezaji mwenzake Derrick Jones walifanya kamari mara kadhaa kwenye mechi za soka, zikiwemo mechi zilizohusisha timu zao wenyewe katika misimu ya 2024 na 2025.
Kwa mujibu wa taarifa ya ligi, katika tukio moja Oktoba 19, 2024, wachezaji hao waliweka dau kwamba Jones angepata kadi ya njano katika mchezo kati ya Columbus Crew na New York Red Bulls – jambo ambalo baadaye lilitokea uwanjani.
Kamishna wa MLS, Don Garber, alisema ligi hiyo imechukua hatua kali kulinda uadilifu wa mchezo na kupinga vikali aina yoyote ya kamari inayohusisha mechi au wachezaji wa ligi hiyo
Ingawa uchunguzi haukupata ushahidi kwamba matokeo ya mechi yalipangwa, MLS ilisema ukiukwaji wa sera ya kamari ni mkubwa na hivyo kuamua kuwafungia wachezaji hao maisha kushiriki mashindano ya ligi hiyo.
