Dereva Boda Boda Ahukumiwa Kunyongwa Kwa Kosa la Kumuua Mtoto Wake

Dereva Boda Boda Ahukumiwa Kunyongwa Kwa Kosa la Kumuua Mtoto Wake
Dereva Boda Boda Ahukumiwa Kunyongwa Kwa Kosa la Kumuua Mtoto Wake

Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imemhukumu kunyongwa hadi kufa Joseph Mhulilwa, Dereva Bajaji na Mkazi wa Mtaa wa Mwalukosi, Mtwivila B, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi mtoto wake wa kumzaa, Timothy Mhulilwa (4), akidaiwa kutenda kitendo hicho kwa lengo la kujipatia utajiri.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Angaza Mwipopo katika kesi namba 25532 ya mwaka 2025, akieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa Mahakamani ulithibitisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Mahakama, tukio hilo la kikatili lilitokea Aprili 12, 2025 ambapo Mshtakiwa alimuua mtoto wake kisha kuukatakata mwili vipande vidogo na kuvitupa kwenye shimo la choo.

Akisoma maelezo ya ushahidi, Jaji Mwipopo alisema mshtakiwa alikiri kuukata mwili wa mtoto vipande na kuponda mifupa mikubwa kwa jiwe ili iwe rahisi kutupwa shimoni.

Baada ya kukamatwa, mabaki ya mwili yalipatikana katika tenki la maji taka na kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba (DNA) uliothibitisha kwa asilimia 99 kuwa yalihusiana na Marehemu na baba yake.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi 13 ambao ushahidi wao uliisaidia Mahakama kufikia uamuzi wa kumtia hatiani Mshtakiwa na kumhukumu adhabu ya kifo kwa kunyongwa.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Geoffrey Mwakasege, alipinga hukumu hiyo akidai mahakama haikuzingatia ipasavyo baadhi ya vielelezo muhimu ikiwemo ramani ya eneo la tukio, ripoti ya uchunguzi wa DNA pamoja na maelezo ya onyo ya mshtakiwa.

Related Posts