
Wanaanga wanne wameanza safari ya kurejea Duniani kwa kutumia chombo cha anga za juu Artemis II baada ya kufanikiwa kufika Mwezini na kushuhudia matukio ya kipekee.
Safari hiyo imeingia katika historia, huku wanaanga hao kutoka Marekani na Canada wakifanikiwa kuona kwa mara ya kwanza kwa macho yao sehemu ya Mwezi ambayo haijawahi kuonwa na binadamu.
Kamanda wa ujumbe huo, Reid Wiseman, alieleza kuwa walishuhudia mandhari zisizo za kawaida walipokuwa wakipita karibu na Mwezi. Naye rubani Victor Glover alisema hakuna maneno yanayoweza kuelezea uzuri na upekee wa walichokiona.
Wanaanga hao walielezea tukio hilo kuwa ni la ajabu na la kushangaza, wakibainisha kuwa uzoefu huo ni wa kipekee katika historia ya uchunguzi wa anga, hasa ikizingatiwa kuwa Mwezi una pande mbili na baadhi ya maeneo yake hayajawahi kushuhudiwa moja kwa moja na binadamu.
Katika kipindi cha saa saba za uchunguzi, waliendelea kutuma taarifa na data mbalimbali Duniani, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa wa kisayansi kuhusu Mwezi.
Aidha, walipokea simu ya pongezi kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, aliyewapongeza kwa ujasiri na mafanikio yao katika safari hiyo muhimu ya kihistoria
