
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, akiwa gerezani Ukonga, amekutana na Rais wa zamani wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera, ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Jumuiya ya Madola, katika mazungumzo yaliyogusa masuala muhimu ya demokrasia, utawala wa sheria na mwenendo wa kesi zinazoendelea nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya CHADEMA, iliyotolewa leo Aprili 16,2026 Lissu alimueleza Chakwera kuwa kesi ya uhaini inayomkabili inatokana na msimamo wake wa “No Reforms, No Election,” akisisitiza haja ya kufutwa kwa kesi zote dhidi yake na chama chake ili kuwezesha mazingira ya ushiriki wa kisiasa akiwa huru.
Katika mazungumzo hayo, Lissu pia alitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa kupitia taasisi za kikanda kama SADC (Jumuiya Maendeleo ya Kusini mwa nchi za Afrika) kuhusu matukio ya Oktoba 2025 kabla na baada ya uchaguzi, pamoja na kuimarishwa kwa uwajibikaji wa taasisi za uchaguzi na usimamizi wa mawasiliano, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume Huru y Mamlaka ya Mawasiliano Tanzaniaa Taifa ya Uchaguzi (INEC) na TCRA.
Aidha, kiongozi huyo wa upinzani alisisitiza umuhimu wa mageuzi ya vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume mbalimbali za kitaifa, pamoja na mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.
CHADEMA imesema Lissu pia amepata nakala ya uamuzi wa Mahakama ya Rufani ulioruhusu chama hicho kuendelea na shughuli zake, ambapo alitoa wito kwa wanachama kujiandaa na hatua zinazofuata za kisiasa, akisisitiza umuhimu wa mikutano ya hadhara katika kuimarisha demokrasia.

