Jinamizi la kujiuzulu lamuandama Rais Ramaphosa


KIONGOZI wa upinzani nchini Afrika Kusini, Julius Malema, amemtaka Rais Cyril Ramaphosa ajiuzulu kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba uliobaini kuwa Bunge lilikiuka Katiba kwa kuzuia mchakato wa kumwondoa madarakani mwaka 2022.

Uamuzi huo umetokana na kesi iliyofunguliwa na chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Malema pamoja na washirika wake, na unaweza kufungua njia ya kuanzishwa upya kwa mchakato wa kumvua madaraka dhidi ya rais huyo.

Ofisi ya Ramaphosa imesema inaheshimu uamuzi wa mahakama.

Mwaka 2022, jopo huru la uchunguzi lilibaini kuwa rais huenda akawa na maswali ya kujibu baada ya dola 580,000 taslimu kuibiwa nyumbani kwake kijijini, fedha zilizokuwa zimefichwa kwenye sofa. Tukio hilo lilizua maswali kuhusu chanzo cha fedha hizo, madai ambayo Ramaphosa ameyapinga.

Hata hivyo, Bunge lilizuia mchakato wa kumwondoa madarakani kupitia kura miaka minne iliyopita, wakati chama chake cha African National Congress (ANC) kikiwa na wingi wa wabunge. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2024, ANC sasa inaongoza serikali ya mseto.

Kufuatia uamuzi wa mahakama, ofisi ya rais imesema Ramaphosa “anaimarisha dhamira yake kwa Katiba, uhuru wa mahakama na utawala wa sheria,” akisisitiza kuwa amekuwa akishirikiana kikamilifu na uchunguzi wote unaohusiana na suala hilo.

“Rais Ramaphosa anaamini kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba tuhuma zozote lazima zichunguzwe kwa haki na kwa kuzingatia taratibu za kisheria,” imesema taarifa hiyo.
Akizungumza nje ya mahakama mjini Johannesburg, Malema amesema rais anapaswa kujiuzulu ili ajikite katika mchakato wa kuondolewa madarakani, akionya kuwa mchakato huo una athari kubwa binafsi na kisiasa.

EFF ilifungua kesi hiyo katika Mahakama ya Juu zaidi mwaka 2024, kwa kushirikiana na vuguvugu la African Transformation Movement.

Malema, ambaye pia anakabiliwa na rufaa katika kesi tofauti inayohusu kumiliki bunduki kinyume cha sheria na kuifyatua hadharani, amesema wabunge wa ANC huenda wakaiunga mkono hatua ya kumwondoa madarakani Ramaphosa iwapo ushahidi utawekwa wazi.

Chama chake pia kimemuandikia Spika wa Bunge la Taifa, Thoko Didiza, kikitaka maelezo ndani ya saa 48 kuhusu hatua zitakazochukuliwa kufuatia uamuzi huo, kwa mujibu wa taarifa ya News24.

BBC

Related Posts