
Iran imepanua mashambulizi yake ya kijeshi katika eneo la Ghuba baada ya kurusha makombora na droni kuelekea Qatar, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) siku ya Jumapili, saa chache baada ya Marekani kufanya duru ya tatu ya mashambulizi ya anga dhidi ya malengo ya Iran.
Milipuko ilisikika katika mji mkuu wa Qatar, Doha, huku mifumo ya ulinzi wa anga ikifanikiwa kuyadungua baadhi ya makombora. Wakazi walitumiwa tahadhari kupitia simu zao wakitakiwa kubaki majumbani.
Nchini Bahrain, ving’ora vya tahadhari vililia katika maeneo mbalimbali, ikiwemo karibu na makao ya Jeshi la Wanamaji la Marekani (US Fifth Fleet), huku UAE nayo ikitoa tahadhari ya mashambulizi ya makombora na droni. Kufikia sasa, mamlaka hazijatangaza idadi ya waliojeruhiwa au maeneo yaliyopigwa.
Mashambulizi hayo yamekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya muda na Iran “yamekufa,” huku akisisitiza kuwa Marekani bado iko tayari kwa mazungumzo ya kufikia suluhisho la kudumu.
Jeshi la Marekani lilisema lilifanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kushambulia meli ya mizigo iliyokuwa ikipitia Mlango wa Hormuz, hatua iliyosababisha uharibifu mkubwa wa chumba cha injini na kuripotiwa kutoweka kwa mfanyakazi mmoja wa kiraia.
Iran nayo ilitangaza kuwa Mlango wa Hormuz utaendelea kufungwa hadi itakapotolewa taarifa nyingine, huku ikionya kuwa inaweza kushambulia vituo vingine vya kijeshi vya Marekani katika eneo hilo ikiwa mashambulizi dhidi yake yataendelea.
Mlango wa Hormuz ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani, ambapo takribani asilimia 20 ya biashara ya mafuta na gesi hupita katika eneo hilo. Kufungwa kwa njia hiyo tayari kumeibua hofu ya athari kubwa kwa uchumi wa dunia na soko la nishati.
Mashambulizi ya Iran pia yamezua kulaaniwa vikali na mataifa ya Ghuba na Mashariki ya Kati, yakiwemo Saudi Arabia, Qatar, UAE na Misri, ambayo yamezitaka pande zote kujizuia na kurejea mezani kwa mazungumzo ili kuzuia mgogoro huo usizidi kuenea.
