
Mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu amefariki dunia, huku mama yake, Selina Qarabas (39), akijeruhiwa mikononi baada ya kushambuliwa na fisi katika Kijiji cha Lambo, Kitongoji cha Haeda, Kata ya Masakta, Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara.
Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo lilitokea usiku wa Julai 14, 2026, wakati Selina alipokuwa akiwafuata watoto wake waliokuwa wamekwenda kusaga nafaka karibu na makazi yao. Wakati huo alikuwa amembeba mtoto mgongoni kabla ya kushambuliwa ghafla na fisi.
Katika harakati za kumzuia mnyama huyo, Selina alipambana naye na kuomba msaada, lakini fisi alifanikiwa kumng’oa mtoto kutoka mgongoni mwake na kutoweka naye.
Mtoto huyo baadaye alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata katika shambulio hilo.
Selina alipata majeraha mikononi wakati wa mapambano na kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, huku hali yake ikiendelea kufuatiliwa na wahudumu wa afya.
Tukio hilo limewaacha wakazi wa Kijiji cha Lambo wakiwa na hofu, wakiiomba Serikali na mamlaka zinazohusika kuchukua hatua za haraka kudhibiti wanyama wakali wanaovamia makazi ya wananchi ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia.
