
Magori Afichua Siri: Kwa Nini Simba Walijitoa Dili la Selemani Mwalimu Aliyeibukia Yanga
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescentius Magori, ameweka wazi sababu zilizowafanya ‘Wekundu wa Msimbazi’ kujiondoa kwenye mbio za kumsajili mshambuliaji Selemani Mwalimu, ambaye hatimaye ametambulishwa rasmi na watani zao wa jadi, Yanga SC.
Magori ameeleza kuwa kilichokwamisha mchakato huo ni mabadiliko ya ghafla ya masharti ya kifedha kutoka kwa klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, inayommiliki mchezaji huyo.
Gharama Kupanda Ghafla Magori alibainisha kuwa Mwalimu alikuwa tayari amewasili nchini na kujiunga na kambi ya Simba, lakini mambo yalibadilika baada ya Wydad kuongeza matakwa mapya ya kifedha.
“Baada ya mchezaji kuingia kambini kwetu, Wydad walibadili msimamo na kutaka Shilingi bilioni 1 kwa ajili ya mkataba wa mkopo wa msimu mmoja pekee. Walidai wamepokea ofa kubwa zaidi kutoka sehemu nyingine,” alisema Magori.
Uamuzi wa Kulinda Uchumi wa Klabu Magori alisisitiza kuwa uongozi wa Simba uliamua kujitoa ili kulinda ustawi wa kifedha wa klabu hiyo, kwani haikuwa na maana kutoa kiasi kikubwa namna hiyo kwa mchezaji anayekuja kwa mkopo wa muda mfupi.
“Huwezi kutoa Shilingi bilioni moja kwa mchezaji wa mkopo wa mwaka mmoja tu. Ni lazima tuheshimu thamani ya fedha. Hatuwezi kufanya maamuzi ya kuwafurahisha watu kwa siku mbili kisha klabu ikaja kupata matatizo na kufungiwa na FIFA baadaye,” aliongeza.
Ujumbe kwa Wanasimba Kuelekea msimu mpya wa 2026/27, Magori amewatoa hofu mashabiki wa Simba na kuwahakikishia kuwa timu yao ipo imara na inaendelea na mchakato wa kushusha vyuma vingine kabla ya dirisha kufungwa Agosti 15, 2026.
