
Rais Samia aomboleza kifo cha Mama Fatma Karume
Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Mama Fatma Karume, mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, aliyefariki dunia Jumatatu, Septemba 21, 2026.
Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mama Fatma, akieleza kuwa kifo chake ni pengo kwa familia na Taifa kwa ujumla.
“Mama Fatma Karume alikuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar, hususan katika vipindi vya harakati za kupigania uhuru, Mapinduzi ya Zanzibar na kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Amesema Taifa litaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wa Mama Fatma katika kuhifadhi kumbukumbu na urithi wa Taifa, pamoja na kuchochea maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Rais Samia ametuma pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, familia ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, ndugu, jamaa na marafiki, pamoja na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kufuatia msiba huo
