
Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga kimefanya uamuzi mgumu wa kubariki kusitishiwa mkataba kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Manqoba Mngqithi na benchi lake.
Kikao hicho kilichofanyika usiku huu kwa njia ya mtandao, kimetoa uamuzi wa mwisho ambao ni kocha huyo kupewa mkono wa kwaheri ikiwa ni saa chache tangu Yanga ipate sare ya kwanza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ugenini dhidi ya TRA United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, leo Jumamosi, Oktoba 24, 2026.
Mbali na uamuzi huo kikao hicho kimeitaka sekretarieti ya Yanga kuanza mchakato wa haraka wa kutafuta kocha mpya atakayechukua nafasi ya raia huyo wa Afrika Kusini.
Muda mfupi uliopita uamuzi huo tayari umemfikia kocha Manqoba ambaye katika kikao cha timu hiyo kilichofanyika usiku huu jijini Arusha, amewaaga wachezaji wake akiwatakia kila la kheri.
Wakati wowote kutoka sasa Yanga itatoa taarifa kamili juu ya uamuzi huo mgumu unaokuja baada ya timu hiyo kuangusha pointi tano katika mechi nane ilizocheza hadi sasa.
Presha kwa Manqoba zilianza kuwa kubwa tangu Yanga ilivyopoteza kwa kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Watani wao wa Jadi, Simba, katika mechi ya Ligi Kuu, Oktoba 10 mwaka huu.
Kiwango duni ambacho Yanga ilikionyesha kwenye mechi hiyo kilionekana kutowavutia wengi na kelele za kundi kubwa la mashabiki wa timu hiyo kutaka aondolewe zilianza.
Hatimaye sare ya bila kufungana dhidi ya TRA United imehitimisha kibarua cha kocha huyo Jangwani.
Manqoba anaondoka akiwa ameiachia Yanga taji moja ambalo ni la Ngao ya Jamii aliloshinda baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba
