
Trump Amsifu Nicki Minaj Jukwaani, Kauli Yake Yazua Shangwe Michigan
Rais wa Marekani, Donald Trump, amezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoa kauli kuhusu umbo la rapa maarufu Nicki Minaj wakati wa mkutano wa kampeni za Chama cha Republican uliofanyika Port Huron, Michigan, Jumapili, Oktoba 25, 2026.
Trump alitoa kauli hiyo alipokuwa akilihutubia kundi la wafuasi wake, kabla ya kumkaribisha Minaj jukwaani, ambapo alimsifia kwa maneno yaliyosababisha umati wa watu kushangilia.

Akizungumza mbele ya wafuasi wake, Trump alirejelea maoni yake ya awali kuhusu umbile la Seneta wa Republican kutoka Ohio, Jon Husted, kabla ya kuhamishia mazungumzo yake kwa Minaj.
“Kwa njia, nililitazama umbo moja la kuvutia sana hapo awali Nicki Minaj,” alisema Trump, kauli iliyopokewa kwa shangwe na umati. Baadaye alimtaka rapa huyo kusimama na kuongeza kuwa ni vigumu kutomwona.
Trump pia alieleza matumaini yake kuwa Minaj hakuudhika na kauli hiyo, akisisitiza kuwa anampenda na kwamba rapa huyo amekuwa akimuunga mkono kwa muda mrefu.
Baada ya Minaj kumaliza kuzungumza na hadhira, Trump aliendelea kumsifia, akisema ni mrembo zaidi na mwanamke mwenye akili.
NICKI MINAJ ATOA SAPOTI KWA TRUMP
Minaj, mwenye umri wa miaka 43, alitumia nafasi yake katika mkutano huo kueleza wazi kumuunga mkono Trump, huku akiwa amevalia suti ya rangi ya dhahabu yenye nembo ya Gucci.
Akizungumza jukwaani, alisema anajivunia kufanya kazi na Rais huyo, akimtaja kama kiongozi anayewakilisha uvumilivu na uwezo wa kusimama tena baada ya changamoto.
Rapa huyo aliongeza kuwa kurejea kwa Trump madarakani kumebadilisha hali ya nchi na kuwapa Wamarekani matumaini mapya kwa ajili yao na watoto wao.
Pia aliwahimiza wapiga kura kuwaunga mkono wagombea wa Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula unaotarajiwa kufanyika Novemba 3, 2026, akisema uchaguzi huo ni kipindi muhimu kwa mustakabali wa Marekani.
JE, NICKI MINAJ ANAWEZA KUJIUNGA NA IKULU YA WHITE HOUSE?
Ushiriki wa Minaj katika mkutano huo umeibua pia mijadala kuhusu uwezekano wa rapa huyo kupewa nafasi ndani ya utawala wa Trump.
Kabla ya mkutano huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa White House, Steven Cheung, alichapisha video iliyomuonyesha Minaj akiwa ndani ya ndege ya rais, Air Force One, akizungumzia sababu zinazomfanya aamini kuwa uchumi wa Marekani unafanya vizuri chini ya uongozi wa Trump.
Cheung aliambatanisha video hiyo na ujumbe wa utani uliodokeza kuwa huenda rapa huyo akawa msemaji mpya wa Ikulu ya White House.
Hata hivyo, ujumbe huo haukuwa tangazo rasmi la uteuzi wake katika nafasi hiyo.
Kauli za Trump kuhusu Minaj na uungwaji mkono wa rapa huyo kwa rais zimeongeza mjadala kuhusu uhusiano kati ya watu mashuhuri katika burudani na siasa za Marekani, hasa wakati nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi muhimu wa katikati ya muhula.
Global Publishers
