
Pigo Yanga: Maxi Nzengeli Aumia Goti, Klabu Yasubiri Majibu ya Vipimo
Dar es Salaam – Klabu ya Young Africans (Yanga SC) imethibitisha kuwa kiungo wake mshambuliaji tegemeo, Maxi Mpia Nzengeli, amepata jeraha la goti na kwa sasa yupo chini ya uangalizi wa madaktari akifanyiwa vipimo vya kina ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu sababu za nyota huyo kutokuonekana kambini, Afisa Habari wa Yanga SC, Ally Kamwe, ameeleza kuwa Nzengeli alipata maumivu hayo wakati wa mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu ya NBC.
Kauli ya Ally Kamwe Kuhusu Hali ya Nzengeli
Kamwe amebainisha kuwa uongozi na benchi la ufundi wanasubiri ripoti rasmi ya kitabibu ili kujua mpango wa matibabu na muda halisi ambao mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja.
“Maxi Nzengeli alipata shida ya goti lake kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi na yupo kwenye vipimo. Hivi karibuni tutajua ripoti kamili baada ya vipimo kufanyika na kubaini ukubwa wa jeraha lake na kama atarejea, atarejea lini,” alisema Ally Kamwe.
Mpango wa Matibabu Kabla Ligi Haijarejea
Afisa Habari huyo aliongeza kuwa klabu imeamua kutumia kipindi hiki cha mapumziko mafupi kuhakikisha kiungo huyo anapata huduma zote muhimu ili aweze kupona kwa wakati.
“Tuliona hizi siku 10 madaktari wake wamuweke sawa na kama matibabu yapo, yafanyike haraka iwezekanavyo ili arejee haraka punde Ligi itakaporudi,” alifafanua Kamwe.
Kwa sasa, muda kamili wa Maxi Nzengeli kurejea dimbani bado haujajulikana, huku mashabiki wa Wananchi wakisubiri kwa hamu taarifa rasmi ya madaktari kuhusu maendeleo ya nyota wao huyo.
