Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joshua Nassari, ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu, Juni 30, 2025, amechukua fomu ya kuwania ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu hiyo, Nassari amesema kuwa uamuzi wake wa kurejea kugombea nafasi hiyo umetokana na ujasiri alionao wa kuwasemea wananchi, uwezo wa kujenga hoja zenye mashiko, uwezo wa kuunganisha watu bila kujali vyama, dini wala itikadi zao, pamoja na kuaminika kwake serikalini kutokana na uzoefu wa kutumikia katika wilaya nne tofauti akiwa kama Mkuu wa Wilaya.
Zoezi la uchukuaji na urudishaji wa fomu kwa ngazi mbalimbali za udiwani na ubunge linaendelea katika ofisi mbalimbali za vyama kote nchini, na linatarajiwa kufungwa rasmi ifikapo Julai 2, 2025.

