Nature
Wachokonozi

Jinsi Vijana Wanaojiita Wachokonozi Walivyoachiwa na Kukamatwa Tena na Polisi

Vijana wawili ambao ni Jackson Kabalo na Joseph Mrindoko wanaounda Kundi la Mtandaoni la WACHOKONOZI, wameachiwa huru katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya upande wa Jamhuri kusema hauna nia ya kuendelea na kesi hiyo lakini wakiwa wanatoka nje ya chumba cha Mahakama hiyo, walikamatwa tena na Polisi na kupelekwa katika Mahakama nyingine ambayo ni ya Wilaya ya Arumeru na kushtakiwa upya kwa makosa mawili.

Mashataka hayo waliyosomewa katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru ni kuchapisha taarifa za uongo kinyume na kifungu namba 16 cha sheria ya makosa ya mtandao na kosa la pili ni kutoa maudhui mtandaoni bila ya kuwa na leseni kinyume na kifungu namba 116(3)(b) cha sheria ya mawasiliano ya kielektroniki na posta.

Mwendesha mashtaka wa Serikali Mahufudhi Mbagwa akiwasomea hati ya mashtaka Watuhumiwa hao katika Mahakama ya wilaya ya Arumeru amesema kuwa kati ya tarehe 23 mwezi wa nne 2025 wakiwa na nia ya kupotosha Jamii walichapisha taarifa ambazo sio kweli kwenye mitandao ya kijamii.

Maelezo ya kosa la pili ni kuchapisha na kusambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, X, Instagram na Youtube bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA kosa wanalodaiwa kulifanya kati ya January 2023 hadi June 2025 ambapo ameeleza kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.

Watuhumiwa wote wawili wameachiwa baada ya kupatiwa dhamana kwa kila mmoja kuwa na Wadhamini wawili na fungu la dhamana la shilingi milioni tatu huku Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo akiiahirisha hadi August 13,2025 ambapo itakuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa

Related Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *