Profesa Adolf Mkenda Atoa Ufafanuzi Kuhusu Kufutwa Baadhi ya Kozi UDOM
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ametoa ufafanuzi kuhusu hatua ya kufutwa kwa baadhi ya kozi za ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambayo imeibua taharuki miongoni mwa wanafunzi na wadau wa elimu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 22, 2025 jijini Dodoma, Prof. Mkenda amesema mabadiliko hayo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha ubora wa walimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanajikita zaidi katika maudhui ya masomo wanayokwenda kufundisha.
“Badala ya kutumia muda mrefu kujifunza namna ya kufundisha, sasa mwanafunzi atatumia muda mwingi kujifunza maudhui ya somo husika, kisha akapate mbinu za kufundishia,” amesema Prof. Mkenda.
Ametolea mfano kozi ya Bachelor of Education in Science and ICT iliyofutwa, akisema kozi hiyo sasa itatolewa kupitia Bachelor of Science with Education, ambayo inalenga kumuwezesha mwanafunzi kusoma kwa kina masomo ya sayansi kabla ya kujifunza mbinu za ualimu.
“Kozi ya awali ilikuwa na maudhui mengi ya Education na kidogo sana kwenye sayansi na ICT. Sasa tumehamia kwenye mfumo ambao mwanafunzi atasoma kwa kina somo analokwenda kufundisha, kisha apate mafunzo ya ualimu kwa ufanisi,” amesema.

